Askari wa Wanyamapori wa Selous wakamilisha mafunzo ya kudhibiti ujangili yaliyotolewa na Wanajeshi wa Kimarekani

Selous Conclusion
Askari wa Wanyamapori wa Selous wakamilisha mafunzo ya kudhibiti ujangili yaliyotolewa na Wanajeshi wa Kimarekani (Picha kwa hisani ya Ubalozi wa Marekani)
Askari wa Wanyamapori wa Selous wakamilisha mafunzo ya kudhibiti ujangili yaliyotolewa na Wanajeshi wa Kimarekani (Picha kwa hisani ya Ubalozi wa Marekani)

Selous Game Reserve, TANZANIA.  Hapo tarehe 27 Machi, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Virginia Blaser, alihudhuria mahafali ya askari wanyamapori wapatao 50 waliohitimu mafunzo ya mwezi mmoja kuhusu mbinu za kukabiliana na usafirishaji haramu wa wanyamapori. Mafunzo hayo yalitolewa na wakufunzi wa Kimarekani kutoka katika kikosi maalumu cha askari wa miguu, wanamaji na wanaanga cha kukabiliana na Majanga Barani Afrika. Mahafali hayo yalihudhuriwa pia na Mkurugezi Msaidizi wa Kudhibiti Ujangili katika Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Faustin Masalu, Kiongozi Mkuu wa Askari wa Wanyamapori katika Hifadhi ya Selous, Bw.  Benson Kibonde na Kanali Phillip Millerd kutoka Jeshi la Marekani.

Katika hotuba yake, Kaimu Balozi Blaser aliwapongeza askari hao kwa kuweza kukamilisha mafunzo hayo magumu na kuwataka kutumia ujuzi walioupata kuwa viongozi bora na mfano wa kuigwa wanapotekeleza wajibu wao wa kulinda urithi wa maliasili za Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa Kudhibiti Ujangili Bw. Masalu alisema kuwa mafunzo na ujuzi ambao askari hao wameupata ni muhimu sana katika kusaidia jitihada za kukabiliana na usafirishaji haramu wa wanyamapori, biashara ambayo imezidi kujiimarisha kimataifa.  “Ushindi dhidi ya vita hii unawezekana kwa kushirikiana na wabia wetu wenye malengo yanayofanana na yetu kama ilivyo kwa Marekani.”

Askari wa Wanyamapori wa Selous wakamilisha mafunzo ya kudhibiti ujangili yaliyotolewa na Wanajeshi wa Kimarekani (Picha kwa hisani ya Ubalozi wa Marekani)
Askari wa Wanyamapori wa Selous wakamilisha mafunzo ya kudhibiti ujangili yaliyotolewa na Wanajeshi wa Kimarekani (Picha kwa hisani ya Ubalozi wa Marekani)

Hii ilikuwa awamu ya kwanza katika mlolongo wa mafunzo yatakayotolewa na askari wa Jeshi la Marekani ili kuwajengea uwezo askari wa wanyamapori wa Hifadhi ya Selous katika kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa wanyamapori.  Mada mahsusi zilizofundishwa katika mafunzo haya zilikuwa ni pamoja na matumizi na usalama wa silaha, ulengaji shabaha, mbinu za doria, mbinu za medani, huduma ya kwanza, kusoma ramani, matengenezo ya magari na misingi ya uendeshaji oparesheni maalumu.  Mafunzo haya yalikamilishwa na mazoezi halisi kwa vitendo ya siku tatu yaliyojumuisha doria zipatazo 25 katika eneo la zaidi ya kilomita 100 za hifadhi.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Japhet Sanga (SangaJJ@state.gov), Afisa Habari Mwandamizi, Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam.