Serikali Ya Marekani Kufadhili Mafunzo Ya Kilimo Kinachoendana Na Hali Ya Hewa

Morogoro. Viongozi na wadau kutoka baadhi ya mikoa na wilaya nchini Tanzania wamekutana Morogoro, Machi 25-29, kwa mafunzo ya Serikali yaliyofadhiliwa na Serikali ya Marekani kuhusu namna ya kupanga mikakati na kusaidia wakulima wadogo ili waweze kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kutekeleza kilimo kinachoendana na hali ya hewa. Mafunzo kama haya yatafanyika Unguja, Zanzibar, Aprili 1-5.

Programu ya mafunzo, “Landscape Climate-Smart Agriculture Pilot Course,” inafanywa na timu ya wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha California, Davis; Idara ya Kilimo ya Marekani (USDA); Chuo kikuu cha Cornell; kampuni ya EcoAgriculture; na Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo (IITA) na fedha kutoka Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).

Mafunzo haya ni sehemu ya Mradi wa kujenga uwezo wa upatikanaji wa Chakula, ambao ni mpango wa Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na USDA na USAID. Mradi huu unaainisha mapungufu ya uwezo wa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi yanayoathiri kilimo. Mradi huu unatekelezwa na IITA, FAO, na World Agroforestry Center.

Kilimo kinachoendana na hali ya hewa kinafafanuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) kama kilimo ambacho huongeza uzalishaji wa chakula na mapato ya wakulima, hupunguza uzalishaji wa gesi zinazochangia ongezeko la joto, na hukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Mbinu hii inasaidia sekta ya kilimo kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na athari zake kwenye hali ya hewa kama ukame, mvua finyu na mafuriko, pamoja na kukidhi ongezeko la mahitaji ya chakula.