Serikali ya Marekani na Tanzania Kushirikiana Katika Kupambana na Aflatoxin kwa kutumia AflasafeTZ

Dar es Salaam, Tanzania — Serikali ya Marekani, kwa ushirikiano na Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo (IITA), inatangaza upatikanaji wa AflasafeTZ, teknolojia yenye ufanisi wa kupunguza ugonjwa wa aflatoxini katika chakula cha binadamu na malisho ya wanyama. Bidhaa hiyo imetengenezwa na IITA na Wizara ya Kilimo Tanzania, kwa ufadhili kutoka Shirika la Marekani la Misaada ya Maendeleo ya Kimataifa (USAID) na Idara ya Kilimo ya Marekani (USDA), baada ya miaka takribani sita ya utafiti nchini.

AflasafeTZ imesajiliwa na Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu kwa nchi za Kitropiki nchini Tanzania, kwa ajili ya kurahisisha utengenezaji na mauzo ya ndani. Itasaidia kupunguza hatari za kiafya kwa binadamu na mifugo na kuepuka athari mbaya za aflatoxins katika biashara na mapato ya wakulima wadogo.

Aflatoxini ni kemikali zenye sumu ambazo huzalishwa na fangasi inayopatikana katika udongo na mabaki ya mazao. Hiyo fangasi inashambulia mazao ya mahindi na karanga, inabaki kwenye mazao baada ya kuvunwa na inaweza kuongezeka na kuzalisha aflatoxini wakati wa kuhifadhiwa, Sumu hii inaweza kusababisha saratani, na kiasi kikubwa kikiingia mwilini, inaweza kusababisha kifo. Hata kiasi kidogo husababisha kinga mwilini kupungua na udumavu kwa watoto. Mifugo inaathiriwa pia, na maziwa yao yanaweza kubeba hiyo sumu na kuathiri watoto wao na binadamu.

AflasafeTz inatumia aina za fangasi ambazo hazitoi sumu ili zizalishwe kwa wingi na kuchukua nafasi ya zile zinazotoa sumu. Kufanya hivi kunapunguza uwepo wa aflatoxini kwenye mahindi na karanga kwa zaidi ya asilimia 80. Teknolojia hiyo ilitengenezwa kwa mara ya kwanza na USDA.