Leo, Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) limeadhimisha mwaka wa kwanza wa mafanikio ya mradi wa USAID Feed the Future Tanzania wa Kilimo Tija katika kijiji cha Ugwanchanya wilayani Iringa.
Hafla hiyo iliyohudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Bw. Peres Magiri, anayekaimu nafasi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bi. Halima Dendego, wawakilishi kutoka USAID, viongozi wa Serikali ya Tanzania, wawakilishi wa sekta binafsi na wakulima ilionesha mafanikio ya mradi huo kwa kuwashirikisha vijana katika kilimo cha bustani chenye faida, na umuhimu wa kutumia mbinu bora na tekinolojia pamoja na jamii kupitia ushirikiano na serikali, sekta binafsi na mamlaka za mitaa.
“Bila msaada kutoka sekta binafsi, jumuiya za wakulima, na serikali ya Tanzania, mradi huu wa USAID usingefanikiwa,” alisema Mratibu wa USAID Feed the Future Dk. Tor Edwards. “Ubia wetu unalenga kusaidia biashara ndogo ndogo na za kati 2,500 za Kitanzania (MSMEs) kuwekeza zaidi ya dola milioni 20 na kuzalisha ajira 7,400, hasa kwa vijana.”
Katika mwaka wa kwanza, mradi ulitoa ruzuku 100 zenye jumla ya TZS 727 milioni, ikiwemo zaidi ya TZS 178 milioni kwa walengwa 22 kutoka mkoa wa Iringa. Ruzuku hizi ziliwezesha upatikanaji wa bidhaa kama vile vifaa vya umwagiliaji kwa njia ya matone, pampu za maji, na kreti za kuvuna ili kusaidia biashara na wakulima wadogo wa kilimo cha bustani. Kutokana na hali hiyo, vikundi vinavyoongozwa na vijana kikiwemo Kikundi cha Agrarian cha Kilimo katika kijiji cha Ugwachanya vimefanikiwa kufuata kanuni bora za kilimo, ambazo zimenufaisha kikundi chao na jamii zinazowazunguka.
Lengo la mradi wa USAID Feed the Future Kilimo Tija ni kubadilisha sekta ya kilimo cha bustani nchini Tanzania kuwa kituo chenye nguvu kikanda, kutengeneza fursa za kiuchumi na ajira kwa vijana. Katika kipindi cha miaka mitano cha utendaji (2022-2027), mradi wa Kilimo Tija wenye thamani za dola milioni 38 utalenga mikoa katika Ukanda wa Kukuza Uchumi wa Kilimo Kusini mwa Tanzania, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba. Lengo kuu la mradi huu ni kuongeza fursa za kiuchumi katika mifumo ya soko la kilimo cha bustani, kwa kuzingatia vijana, ukifanya kazi na vyama vya umma na sekta binafsi, taasisi zinazoongozwa na vijana na wanawake, na mamlaka za serikali za kitaifa na za mitaa.