Marekani yashirikiana na Tanzania na Asasi za Kiraia Kuimarisha Utoaji wa Huduma za Afya ya Jamii

Dar es Salaam: Februari 22, 2019, Serikali ya Marekani ilishirikiana na Serikali ya Tanzania na asasi 12 za kiraia ili kuimarisha utoaji wa huduma za afya katika mikoa ya Iringa, Njombe, Morogoro, Lindi na Mtwara. Mchango wa Serikali ya Marekani wa baiskeli 2,160 utaongeza uwezo wa kujitolea kwa wahudumu wa afya kutoa huduma kwa wateja wenye Virusi Vya UKIMWI katika maeneo ya mbali ili kuboresha upatikanaji wa huduma za afya za VVU na huduma za matibabu.

Wakati wa sherehe ya makabidhiano, Kaimu Balozi Patterson alisema, “Ubia wetu ni hatua muhimu katika kusaidia kuziwezesha jamii kukabiliana na vikwazo vingi zaidi vya kuboresha afya zao. Watasaidia Serikali ya Marekani na wabia wetu wa Tanzania kufikia lengo letu la pamoja la kuboresha upatikanaji wa huduma za afya muhimu kusini mwa Tanzania. ”

Serikali ya Marekani inafanya kazi na Serikali ya Tanzania, asasi za kiraia, na jamii ili kuongeza upatikanaji wa huduma bora za afya, zilizo jumuishi, hasa kwa wanawake na vijana, kuboresha hadhi ya afya ya Watanzania wote. Serikali ya Marekani inajivunia kuwa na ubia na Serikali ya Tanzania na asasi za kiraia katika kuzuia, kugundua, na kukabiliana na kuzuka kwa magonjwa hatari ya kuambukiza, wakati huo huo kusaidia watu wa Tanzania na nchi nyingine za Afrika wakiwa na jitihada zao wenyewe.

Serikali ya Marekani ilifadhili mchango huu kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) na mradi wake wa Boresha Afya wa Kanda ya Kusini na ufadhili kutoka kwenye Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa UKIMWI (PEPFAR).