Serikali Ya Marekani Yatoa Fedha Kuunda Biashara Na Ajira Kwaajili Ya Vijana Wa Vijijini

Iringa, Tanzania – Oktoba 31, 2018, Terhi Majanen, Mkurugenzi wa Shirika la Marekani la Misaada ya Maendeleo ya Kimataifa Ofisi ya Kukuza Uchumi Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam, alitoa misaada sita yenye thamani ya Dola za Kimarekani 527,000 kwa biashara ndogo ndogo na mashirika binafsi kutoka Iringa, Mbeya na Zanzibar.

Mradi wa Kuinua Vijana wa Ubalozi wa Marekani unasaidia shughuli zinazowawezesha vijana wenye umri wa miaka 15-35 katika maeneo ya vijijini nchini Tanzania kuongeza uwezo wao wa kuajirika, uelewa wa biashara, ujuzi wa uongozi, ustadi wa afya na ushiriki katika maisha ya kiraia.

Misaada hiyo inatarajiwa kuunda ajira zaidi ya 700 na kuanzisha na kuboresha makampuni ya biashara zaidi ya 500 yakiongozwa na vijana. Fedha zitatumika kuwapatia vijana mafunzo ya ujasiriamali na fursa, na kuboresha upatikanaji wa fedha, ujuzi na usimamizi wa fedha, na utayari wa kazi. Hii itawawezesha vijana kuanzisha au kupanua biashara au kuchukua nafasi ya fursa za kazi katika kilimo na sekta zinazohusiana.