Serikali ya Marekani Yatoa Misaada Yenye Thamani ya Dola 750,000 Ili Kutengeneza Ajira Kwa Vijana wa Vijijini

Mbeya, Tanzania – Mei 29, 2019, Serikali ya Marekani ilitoa misaada yenye thamani ya dola 750,000 kwa taasisi tisa ambazo zinasaidia utengenezaji wa ajira, ujasiriamali, uongozi, na maisha bora kwa vijana. Misaada hiyo inatolewa na mradi wa Inua Vijana wa Feed the Future Tanzania , inayofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), na wanatarajia kutengeneza ajira 950 kwa vijana katika makampuni 700 mapya au ambayo yanaongozwa na vijana katika mikoa ya Iringa, Mbeya, na Zanzibar.

Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Andrew Karas, na Mheshimiwa Suleiman Jafo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), walikabidhi misaada hiyo kwa taasisi husika.

Wakati wa hotuba yake, Bwana Karas alibainisha kuwa “Kuwekeza katika uongozi wa vijana nchini Tanzania ni kipaumbele cha USAID na Serikali ya Tanzania. Asilimia kubwa ya Watanzania ni vijana, na idadi ya wananchi wake inatarajiwa kuongezeka mara mbili ndani ya miaka 25 hadi 30 ijayo. Jitihada za makusudi zinahitajika kwa serikali, sekta binafsi na jamii ili kuhakikisha kuwa nguvu, vipaji, na matumaini ya vijana wa leo, pamoja na kizazi kijacho, zinafanya Tanzania kuwa mahali pa mafanikio kwa wote.”

Mradi wa Inua Vijana unahamasisha vijana wa vijijini kushiriki katika sekta ya kilimo nchini Tanzania na kuwapatia fursa za kiuchumi vijana wenye umri wa miaka 15-35 pamoja na kuhamasisha uongozi na mienendo ya kiafya. Kupitia misaada hii, Inua Vijana ya Feed the Future Tanzania itabadili changamoto kuwa fursa kwa vijana wa vijijini kuongoza na kushiriki katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.