Serikali ya Marekani yazindua Mradi wa Afya wa Dola Milioni 56 kushughulikia athari za VVU kupitia msaada kwa Watoto, Vijana na Familia zilizo katika mazingira hatarishi
Dodoma – Leo, wawakilishi wa serikali ya Marekani, kupitia Shirika la Marekani la Ushirikiano wa Kimataifa (USAID) na wawakilishi wa serikali ya Tanzania wamesherehekea kuendelea kwa ushirikiano wao katika kuendesha afua za VVU zinazookoa maisha, kwa kuzindua mradi mpya uitwao Kizazi Hodari. Mradi huu wa miaka mitano, wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 56, utatoa huduma za kuzuia maambukizi ya VVU na kuboresha maisha ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na jamii zilizoathiriwa na VVU nchini kote Tanzania.
Tanzania imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI. Toka mwaka 2003, serikali ya Marekani kupitia PEPFAR imetoa zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 6 katika kupambana na virusi hivi na imekuwa mfadhili mkubwa zaidi wa jitihada za kupambana na VVU/UKIMWI nchini Tanzania. Leo hii, zaidi ya Watanzania milioni 1.5 wanaoishi na VVU wanapata matibabu ya kufubaza VVU yanayowawezesha kuishi maisha marefu na yenye afya. Hata hivyo, lengo la kutokomeza kabisa VVU linakabiliwa na changamoto kubwa ya watu wengi kutokujua hali zao za maambukizi ya VVU; asilimia ndogo ya watu wanaoishi na VVU/UKIMWI ambao wapo katika matibabu na kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU miongoni mwa wasichana na wanawake.
Mradi wa Kizazi Hodari unaendeleza mafanikio yaliyofikiwa na mradi mwingine wa USAID uliojulikana kama Kizazi Kipya na mradi unaoendelea wa ACHIEVE, kwa kufanya kazi na serikali ya Tanzania, jamii na vijana katika kutatua changamoto hizi. Kizazi Hodari unalenga kuboresha afya, ustawi na ulinzi kwa yatima, watoto na vijana walio katika mazingira hatarishi hususan katika jamii zenye viwango vikubwa vya VVU. Aidha, mradi huu utaongeza upatikanaji na matumizi ya huduma za afya, kinga dhidi ya VVU, matibabu, ulinzi, elimu na huduma nyingine za kijamii na kiuchumi miongoni mwa yatima na watoto na vijana walio katika mazingira hatarishi.
Akizungumza Wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkazi wa USAID V. Kate Somvongsiri alisema, “Ili kufikia lengo la kulidhibiti janga hili, ni lazima sisi sote tuongeze ari na kujitoa kwetu katika kuimarisha mifumo ya afya ya Tanzania na kuongeza jitihada za kuutokomeza ugonjwa huu unaosababisha vifo. Mradi wa Kizazi Hodari, ambao unazilenga familia na kumuweka mtoto kama kitovu cha shughuli zake za kuboresha afya, usalama, elimu na utulivu, ni sehemu muhimu ya jitihada hizi. Tunafahari kuwa sehemu ya jitihada hizi muhimu.”