Flag

An official website of the United States government

Serikali ya Marekani Yazindua Mradi wa dola milioni 10.6 Kuwezesha Vijana wa Kitanzania
3 MINUTE READ
Febuari 23, 2023

Zanzibar – Wawakilishi kutoka serikali ya Marekani, na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar walikusanyika katika viwanja vya Maisara mjini Zanzibar kwa ajili ya uzinduzi wa mradi mpya unaolenga vijana wenye thamani ya dola milioni 10.6. Mradi huu wa Kijana Nahodha ni wa miaka minne wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID),unalenga kutoa ujuzi kwa vijana wa kitanzania na kuwasaidia kuwa mawakala wa kuleta mabadiliko katika jamii zao. Kijana Nahodha utatekelezwa na T-MARC, asasi ya wazawa isiyo ya kiraia katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Zanzibar, (visiwani Unguja na Pemba).

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi akiwa Mgeni Rasmi alizindua mradi huu uliohudhuriwa wa wajumbe kutoka wizara, wawakilishi wa kanda ya Zanzibar, wakala nyingine za serikali, mashirika ya kimataifa ya maendeleo, asasi za kiraia na vijana kote Zanzibar.

USAID Kijana Nahodha ni mradi wa sekta mtambuka unaofanya kazi katika sekta ya ajira, elimu, kilimo, utawala bora na afya, na unalenga kujenga uwezo wa vijana wenye umri kati ya miaka 15-25. Kujenga uwezo huu ni pamoja na kuongeza upatikanaji na ubora wa stadi mbalimbali; mafunzo ya ufundi; kuboresha uelewa wa afya ya akili kupitia zana za elimu ya kidijitali zinazoongozwa na watu binafsi; na kuimarisha njia za wazi za mawasiliano kati ya vijana na serikali za mitaa ili kuinua sauti za vijana katika maisha ya kiraia, siasa, na utungaji sera.

Akizungumza katika hafla hii, Mkrurgenzi Mkazi wa USAID V. Kate Somvongsiri alisema, “ Kupitia Kijana Nahodha, tunalenga kuwawezesha vijana kupitia ujuzi mbalimbali; maarifa sahihi ya kuendesha biashara; msaada kutoka kwa familia zao, jamii, na serikali; ili wapate fursa kupitia elimu na ujuzi.”

Mradi wa Kijana Nahodha unatarajia kuwawezesha vijana zaidi ya 45,000 – takribani 10,000 kutoka Zanzibar na 35,000 katika mikoa miwili iliolengwa ya Bara.