Shaambulio kwa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO)

Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Heather Nauert
Msemaji wa Wizara wa Mambo ya Nje
Washington, DC
8 Disemba, 2017

Marekani inalaani vikali shambulio la usiku wa jana dhidi ya vikosi vya kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO) ambapo walinda amani 14 wa Kitanzania walipoteza maisha na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa, ikiwa ni pamoja na askari watano wa Jeshi la DRC. Tunatoa rambirambi zetu za dhati kwa familia ya askari waliopoteza maisha, serikali ya Tanzania , Serikali ya DRC na kwa MONUSCO. Aidha, tunawatakia majeruhi wote kupona haraka.

Umoja wa Mataifa umelielezea hili kuwa shambulizi baya zaidi kufanywa dhidi ya walinda amani katika historia ya hivi karibuni. Marekani inasisitiza kuwa walinda amani si sehemu ya mgogoro na hawapaswi kuwa walengwa wa mashambulizi yoyote. Hivyo basi, mashambulizi haya ya maksudi hayakubaliki. Tunatoa wito kwa serikali ya DRC kufanya uchunguzi wa kina kuhusu shambulizi hili na kuhakikisha kuwa wale wote waliohusika wanafikishwa katika vyombo vya sheria.

Marekani inaendelea kusisitizia dhamira yake ya dhati ya kuisaidia MONUSCO katika jitihada zake za kuwalinda raia dhidi ya mashambulizi na utumiaji mabavu, kuzuia uhalifu na kusaidia kurejesha amani na utulivu nchini DRC. Aidha, tunatoa shukrani zetu za dhati kwa wanaume na wanawake jasiri wanaohudumu katika vikosi hivyo vya kulinda amani.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Ofisi ya Habari ya Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam kwa simu namba: +255 22 229-4000 au kwa barua pepe:  DPO@state.gov.