Jana Tanzania ilimpoteza mmojawapo wa majabali (wa kisiasa). Kwa niaba ya Rais Biden, Serikali ya Marekani, na watu wa Marekani, ninatoa rambirambi zangu za dhati kwa Watanzania wote kwa kuondokewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad.
Seif alijulikana sana kwa jina la “Maalim,” jina lililoenzi taaluma yake kama “Mwalimu.” Hakika jina hilo lilisadifu haiba na matendo yake, kwani alikuwa na mengi ya kutufundisha.
Maalim Seif hakutaka kuwa mwanasiasa, lakini alitumia zaidi ya miaka 40 katika siasa. Alichaguliwa na wengine kuongoza kutokana na karama kubwa alizojaaliwa: huruma yake, busara yake na msimamo wake thabiti. Historia yake inatueleza kuwa aliingia serikalini akitokea shule ya sekondari, baada ya kuombwa na Serikali mpya ya Mapinduzi ya Zanzibar kujaza nafasi ya utumishi wa umma iliyokuwa imeachwa wazi. Hali hii imekuwa ikijirudia katika miongo yake yote ya kuwatumikia watu wa Zanzibar, ikiwa ni pamoja na katika siku za mwisho za utumishi wake, pale Rais Mwinyi alipomuomba kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Katika mkutano wangu na Maalim Seif niliguswa sana na ukimya na utaratibu wake, lakini uliohifadhi ndani yake ushupavu na ujasiri mkubwa. Ameonyesha ujasiri huo mara nyingi wakati wote wa utumishi wake, wakati mwingine akifanya kazi na serikali na wakati mwingine akiipinga, jambo lililomgharimu sana binafsi.
Katika siku zake za mwisho, alifanya vitu viwili vya kijasiri sana. Kwanza, aliunga mkono Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar kwa kuungana na Rais Mwinyi katika jitihada za kutibu majeraha ya kisiasa na kuwa kiongozi wa Wazanzibari wote. Pili, pale alipoumwa Covid-19, aliujulisha ulimwengu kuhusu matokeo ya vipimo vyake, akionyesha kujali na kujitoa kwake katika kulinda afya na usalama wa Watanzania wote.
Katika kuenzi ujasiri wake, katika kuheshimu kumbukumbu yake, yatupasa sote tupite katika njia aliyotuanzishia na kujitahidi kwa kadri ya uwezo wetu kuyaishi yale aliotuachia.
Upumzike kwa amani.