Flag

An official website of the United States government

Tamko la Balozi wa Marekani Donald Wright Kuhusu Kuibuka upya kwa Covid-19 nchini Tanzania
4 MINUTE READ
Mei 18, 2022

26 Februari 2021

Habari zenu. Mimi ni Don Wright, Balozi wa Marekani nchini Tanzania. Ningependa kuzungumza nawe kuhusu janga la COVID-19 na namna ambavyo tunaweza kufanya kazi pamoja kuzuia kuenea kwake na kutusaidia sote kubaki salama.

Toka kuanza kwa janga la Covid-19,  takriban watu milioni mbili na nusu wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huu. Janga hili ni kubwa na hakuna nchi ambayo haijaguswa.

Nchini mwangu, Marekani, tumepoteza raia wenzetu zaidi ya 500,000.  Na kufanya tatizo hili kuwa gumu zaidi, aina mpya ya virusi hivi vimesababisha wimbi kubwa na kali zaidi la maambukizi duniani kote ikiwemo barani Afrika.  Inaonekana wazi kuwa aina hii mpya ya virusi imewasili pia nchini Tanzania.

Nimetiwa moyo sana na matamko yaliyotolewa hivi karibuni na Wizara ya Afya yakiutambua ugonjwa wa COVID-19 kama janga la afya ya jamii nchini Tanzania na kuwataka raia kuchukua hatua za msingi za kujilinda dhidi ya maambukizi: kama vile kuepuka misongamano, kuvaa barakoa na kuacha nafasi inayotakiwa kati ya mtu mmoja na mwingine.  Huu ni ushauri mzuri na ninahimiza kila mmoja aufuate.

Pamoja na kutekeleza hatua hizi za msingi za tahadhari ili kuzuia kuenea kwa COVID-19, kuna angalau zana nyingine mbili ambazo ni muhimu sana katika kudhibiti janga hili.

Mosi, ili kufahamu iwapo hatua zinazochukuliwa zinaleta matokeo yaliyokusudiwa, ni muhimu sana kukusanya na kutoa taarifa na takwimu kuhusu upimaji na visa vya maambukizi. Hii ndiyo sababu ni muhimu sana kwa serikali zote kuwasilisha kwa Shirika la Afya Duniani (WHO) taarifa sahihi, na kwa wakati, kuhusu idadi ya visa katika nchi zao.  Kutoa taarifa hizi kunawahakikishia  raia kuwa serikali zao zinapambana kulinda afya na maisha yao. Isitoshe, utoaji wa taarifa hizo huwawezesha watafiti na wanasayansi kufuatilia vyema zaidi ugonjwa na kuzuia vifo vinavyoweza kuepukika – iwe ndani ya nchi au katika kanda.

Zana ya pili ni chanjo.  Kama alivyosema Waziri wetu mpya wa Mambo ya Nje Tony Blinken, “Hadi pale ambapo kila mmoja duniani atakuwa amechanjwa, basi hakuna hata mmoja atakayekuwa salama kabisa.” Chanjo zimesaidia kutokomeza baadhi ya maradhi mabaya kabisa duniani na hakuna shaka yoyote kwamba kampeni kubwa ya chanjo itaokoa maisha.  Hebu angalia takwimu kutoka Marekani; katika wiki chache tu zilizopita, hasa baada ya mamilioni ya watu kupata chanjo, idadi ya visa vipya vya maambukizi ya Covid-19, idadi ya watu wanaolazwa na idadi ya vifo imeanza kupungua. Ninatoa wito kwa Serikali ya Tanzania kukutanisha wataalamu wake wa afya na kupitia ushahidi kuhusu chanjo.

Ikiwa mtoaji mkubwa zaidi duniani wa misaada ya kiafya na kibinaadamu, Marekani inaendelea kuongoza jitihada za kimataifa dhidi ya janga la Covid-19, ikichangia zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 1.5 katika jitihada za kudhibiti COVID-19 duniani kote na imeahidi kutoa Dola za Kimarekani bilioni 4 ili kuharakisha usambazaji wa chanjo duniani.

Hapa Tanzania, toka kisa cha kwanza cha COVID-19 kiliporipotiwa mwezi Machi 2020, tumetoa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 16.4 ili kukabiliana na janga hili.  Marekani ipo tayari kuongeza zaidi jitihada zetu na tuna dhamira ya dhati ya kufanya kazi bega kwa bega na Tanzania  kuishinda Covid-19.

Ninapenda kumalizia ujumbe huu kwa kuelezea uzoefu wangu binafsi. Mimi ni daktari kwa taaluma. Kabla ya kuteuliwa kuwa Balozi nchini Tanzania, Nilifanya kazi katika sekta ya afya ya umma kwa zaidi ya miaka 30. Ninaweza kuwahakikishia kabisa kwamba hatua za kulinda afya ya umma nilizozizungumzia ZINA UFANISI. Iwapo zitafuatwa na kuzingatiwa zitaokoa maisha. Ninatoa wito kwa Watanzania wote kuungana sasa katika kuunga mkono hatua hizi ili tuweze kulindana na kuwalinda wale tuwapendao.

Asanteni sana.