Pongezi za Balozi Mark B. Childress kwa Bi. Vicky Ntetema kwa kushinda Tuzo ya Kimataifa ya Wanawake Jasiri kwa mwaka 2016

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry na Mkurugenzi Mtendaji wa Under the Same Sun Tanzania Vicky Ntetema baada ya kutunukiwa tuzo ya Wanawake Jasiri wa Kimataifa kwa mwaka 2016 huko Washington, D.C. Marekani, tarehe 29 Machi 2016.

Kwa niaba ya watu wa Marekani, ninapenda kuchukua fursa hii kumpongeza kwa dhati kabisa Bi. Vicky Ntetema, Mkurugenzi Mtendaji wa asasi isiyo ya kiserikali ya Under the Same Sun Tanzania kwa kupokea tuzo ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ya Wanawake Jasiri Kimataifa ya mwaka 2016 iliyotolewa jana jijini Washington.

Sisi katika Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania tulijawa na fahari isiyo kifani kumuona Bi. Ntetema akiwa miongoni mwa wanawake wengine kumi na tatu kutoka pande zote za dunia waliopokea tuzo hii na hasa kuona wakipongezwa na kuenziwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry na Makamu wa Rais Joe Biden.

Kwa muda mrefu nimekuwa nikifahamu kuhusu kazi za utetezi zinazofanywa na Bi. Ntetema na nilipokutana naye wiki iliyopita, nilistaajabishwa sana na weledi, ari na hamasa yake wakati akielezea changamoto zinazowakabili watu wenye albinism.

Aidha, nilivutiwa sana na mafanikio yake.  Kutoka kazi yake kama mwandishi wa habari za kiuchunguzi aliyefichua biashara katili na ya kutisha ya viungo vya miili ya Watanzania wenye albinism hadi jitihada zake za utetezi wa haki za binadamu za watu hao nchini Tanzania na duniani kote, Bi. Ntetema ni mfano kwetu sote wa namna tunavyoweza kusimama kidete na kwa ujasiri dhidi ya udhalimu.

Tunajivunia kufanya kazi na Bi. Ntetema, wabia wetu katika Serikali ya Jamhuri na Muungano wa Tanzania na wananchi wa Tanzania katika kuhakikisha kuwa raia wote bila kujali rangi za ngozi zao wanaishi kwa amani na usalama, mambo ambayo kwayo Tanzania inasifika duniani kote.

Kwa taarifa zaidi kuhusu tamko hili, tafadhali wasiliana kwa barua pepe na Japhet Sanga (SangaJJ@state.gov), Afisa Habari Mwandamizi wa Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam.