Flag

An official website of the United States government

Tamko kuhusu kushambuliwa kwa Freeman Mbowe
2 MINUTE READ
Juni 9, 2020

Ubalozi wa Marekani umestushwa na kuhuzunishwa sana na tukio la kikatili la kushambuliwa kwa Mbunge na Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe hapo tarehe 9 Juni. Ubalozi unatoa wito wa kufanyika haraka kwa uchunguzi wa kina na huru na kisha kukamatwa na kushtakiwa kwa wale wote waliohusika katika shambulio hilo.

Ubalozi unaliona tukio hili katili na lisilo na sababu, la kuvamiwa kwa kiongozi wa upinzani kama tukio la hivi karibuni katika mlolongo mrefu wa matukio ya kusikitisha ya utumiaji nguvu na unyanyasaji yanayofanywa dhidi ya wanachama wa vyama vya upinzani. Aidha, Ubalozi unatambua kuwa mojawapo ya matukio haya ya kikatili ni jaribio la mauaji lililotokea tarehe 7 Septemba 2017 dhidi ya Mbunge na kiongozi wa upinzani Tundu Lissu ambalo ufumbuzi wake haujapatikana hadi leo. Kwa mara nyingine tena tunatoa wito kwa vyombo vinavyohusika kuwabaini, kuwakamata na kuwafungulia mashtaka wale wote waliohusika na tukio hilo.

Ubalozi unatoa pole kwa Mbunge Mbowe na familia yake katika kipindi hiki kigumu na kumtakia apone haraka.