Taarifa kuhusu Mpango wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) nchini Tanzania

Muhtasari: PEPFAR ni mpango maalumu wa Serikali ya Marekani wa kusaidia kuokoa maisha ya watu wanaoishi na VVU/UKIMWI duniani kote.  Mpango huu wa kihistoria ni mkubwa zaidi ya mpango wowote uliowahi kuendeshwa na nchi yoyote duniani katika kukabili ugonjwa mmoja kimataifa.  Mpango wa PEPFAR huongozwa na kuendeshwa na majukumu ya pamoja kati ya nchi wafadhili na nchi wabia na wadau wengine katika kuokoa maisha.

Kupitia PEPFAR, Marekani imesaidia dunia kuwa salama zaidi kwa kupunguza vitisho vya magonjwa ya kuambukiza.  Awali mpango huu ulibuniwa ili kutoa huduma za kuokoa maisha katika nchi zilizokuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU/UKIMWI, hata hivyo hivi sasa PEPFAR inalenga kudhibiti kuenea kwa VVU/UKIMWI duniani kote.  Mpango huu unajumuisha miradi ya Serikali ya Marekani inayolenga afya, maendeleo, usalama na diplomasia ukiwa na uwezo mkubwa wa kufikia malengo na matokeo yaliyo wazi, yanayopimika na yanayobadilisha maisha.

Taarifa na takwimu muhimu kuhusu matokeo ya mpango huu:

  • Katika mwaka wa fedha 2019 pekee, PEPFAR iliwezesha upimaji wa VVU kwa Watanzania milioni 8, huku zaidi ya watu 300,000 waliogunduliwa kuwa na VVU wakiunganishwa na matibabu.
  • Serikali ya Marekani kupitia PEPFAR na Global Fund iliwezesha Watanzania milioni 1.2 kupata matibabu ya kufubaza VVU (antiretroviral treatment).
  • Katika mwaka wa fedha wa 2019, PEPFAR ilitoa matibabu ya kuokoa maisha kwa akina mama wajawazito wapatao 60,000 ili kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
  • Katika mwaka wa fedha 2019, kwa msaada wa PEPFAR, zaidi ya wanaume 780,000 walishiriki katika mpango wa hiari wa tohara kwa wanaume (VMMC)

Miaka 16 toka kuanzishwa kwa PEPFAR hapo mwaka 2003:

  • Vifo vitokanavyo na UKIMWI vimepungua kwa asilimia 80, kutoka vifo 110,000 mwaka 2003 hadi 24,000 mwaka 2018
  • Kiwango cha maambukizi mapya kwa mwaka kimeshuka kwa takriban asilimia 30, kutoka maambukizi mapya 100,000 mwaka 2003 hadi 72,000 mwaka 2018

Mchango wa PEPFAR wa miaka 16 kwa Watanzania unaakisi uhusiano wetu imara na wa muda mrefu na Watu wa Tanzania:

    • Kupitia PEPFAR, Serikali ya Marekani imetumia takriban Shilingi trilioni 9 (Dola za Kimarekani bilioni 5)
    • Fedha zilizotengwa kwa ajili ya mwaka wa fedha 2020 ni zaidi ya Shilingi bilioni 909 (Dola za Kimarekani milioni 395)