Tamko la Masikitiko Kuhusu Chaguzi Ndogo za Agosti 12, 2018

Marekani imesikitishwa na uendeshaji wa chaguzi ndogo zilizofanyika nchini Tanzania tarehe 12 Agosti 2018. Taarifa za kuaminika zinaonyesha kuwa chaguzi ziligubikwa na vurugu zilizohusiana na uchaguzi, ukiukwaji wa sheria za uchaguzi ikiwa ni pamoja na kukataa kwa baadhi ya watendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwasajili wagombea kutoka vyama vya upinzani, vitisho vya polisi dhidi ya wanachama wa vyama vya upinzani, watu kukamatwa kiholela bila kuwepo vibali vya ukamataji na kukandamizwa kwa uhuru wa kukusanyika na kutoa maoni katika kipindi chote kuelekea chaguzi hizo. Mambo haya yanakwaza haki ambazo Katiba ya Tanzania imewapa raia wake na kuhatarisha amani, utulivu na usalama nchini na katika eneo lote la kanda.