Tamko la Ubalozi wa Marekani Kuhusu VVU/UKIMWI nchini Tanzania

Logo - U.S. Embassy Dar es Salaam

Tunatambua kwamba hivi karibuni Serikali ya Tanzania imetangaza mabadiliko katika muongozo wa utoaji huduma za kukabiliana na VVU/UKIMWI kwa makundi maalumu yaliyo katika hatari zaidi ya kuambukizwa VVU na yenye viwango vikubwa zaidi vya maambukizi ya virusi hivyo. Serikali ya Tanzania haijaipatia Serikali ya Marekani taarifa yoyote rasmi kuhusu mabadiliko haya yanayoweza kuathiri programu zinazofadhiliwa na Marekani na kukwamisha maendeleo yaliyofikiwa katika miaka michache iliyopita katika jitihada za kukabiliana na janga la VVU/UKIMWI nchini Tanzania.  Tunaona kwamba uamuzi uliotangazwa na Serikali ya Tanzania wa kupiga marufuku utoaji wa huduma zilizothibitika kuwa na matokeo chanya utasababisha Watanzania wachache zaidi kupata  huduma zitakazookoa maisha yao na kuongeza mlipuko wa ugonjwa miongoni mwa wale wenye mahitaji makubwa zaidi ya kuvidhibiti virusi hivi.

Takwimu zinaonyesha wazi kuwa utoaji wa huduma kwa makundi yaliyo katika hatari zaidi ya maambukizi kwa kupitia miradi ya jamii ya kuwafikia walengwa (community outreach) ikiwa ni pamoja na vituo maalumu vya huduma kwa makundi haya (drop in/resource centers) ni njia yenye ufanisi ya kuyafikia makundi haya na makundi mengine yaliyokatika hatari na yanayokosa huduma za uhakika, ikiwa ni pamoja na vijana ambao kwa ujumla hukosa huduma katika hospitali na vituo vya afya. Marekani inathamini sana ubia wake wa muda mrefu na wenye mafanikio na Tanzania katika sekta ya afya, hususan maendeleo ambayo Tanzania imeyafikia katika jitihada za kukabiliana na VVU/UKIMWI kwa msaada wa Mpango wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR).