Tanzania Njiapanda

Virginia Blaser, Chargé d'Affaires of the United States of America
Virginia Blaser – Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania
Virginia Blaser – Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania

Na Virginia Blaser – Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania
1 Juni 2017

Kwa kipindi cha miaka minne iliyopita nilipata heshima ya kufanyakazi bega kwa bega na Watanzania, Wamarekani na wabia wengine waliojitoa kwa dhati kutekeleza programu na sera zinazoboresha maisha ya mamilioni ya watu nchini na katika kanda. Kuanzia utoaji huduma za afya kwa akina mama wajawazito na kupeleka umeme vijijini – hadi kufanya kazi mashuleni kuboresha elimu ya msingi na kusaidia biashara mpya zinazotoa ajira kwa maelfu ya watu – sote kwa pamoja tumepiga hatua muhimu.

Programu hizi ni sehemu ndogo tu ya ubia wetu mpana ambao umedumu kwa miongo sita sasa. Katika kipindi chote hicho, Tanzania imepitia vikwazo na changamoto mbalimbali – ­na kuzishinda huku Watanzania wakendelea kuwa na tabia na haiba imara na kudumisha mshikamano wao kama jamii. Kwa hakika nikiwa mwanadiplomasia nimejifunza mengi kutokana na umuhimu ambao Watanzania wanauweka katika mashauriano na kufikia mwafaka jambo ambalo kwa miaka mingi limeiwezesha nchi hii kupiga hatua kubwa.

Kwa mtazamo wangu kama mwanadiplomasia niliyehudumu kwa muda mrefu na ambaye ametokea kuipenda nchi hii adhimu, naiona Tanzania leo ikiwa katika njia panda muhimu. Tanzania ina uwezo – na kwa hakika ipo tayari – kupiga hatua kubwa sana kiuchumi na kidemokrasia. Katika njia hiyo naiona nchi ya amani, yenye ustawi, usalama na demokrasia thabiti – ambayo watu wake wana sauti kama wabia muhimu. Nawaona watu wenye kujiamini na kujiona salama wanapotumia sauti yao vyema kuchangia katika jamii yao na maendeleo ya nchi yao. Katika njia hii watu wanashiriki kikamilifu katika nyanja zote za maisha ya umma. Wawekezaji wa nje wana ari ya kuingia ubia na wajasiriamali wa Kitanzania ambao kwa kujiamini kabisa wanaanzisha biashara mpya. Uchumi unakua. Taasisi za Serikali zinaendeshwa kwa uwazi na zinawajibika kwa raia. Shule zinatoa elimu bora kwa wanafunzi wote bila kujali jinsi au asili yao. Kila mmoja ana haki sawa ya kupata huduma za matibabu. Idadi kubwa ya vijana inageuka kuwa mtaji unaozalisha faida kwa vijana hao kupata nafasi za ajira na fursa nyingine mbalimbali. Polisi wanaheshimu utawala wa sheria na haki za raia. Uhuru wa kikatiba, ikiwa ni pamoja na uhuru wa kujieleza na uhuru wa habari  unalindwa, unaheshimiwa na kuhimizwa. Katika mwelekeo huu, uwezo na fursa kubwa ya Tanzania kupiga hatua kubwa unafikiwa kikamilifu.

Hata hivyo katika njiapanda hii, kuna njia nyingine. Njia hii inaielekeza Tanzania mahali ambapo watu wake wanaogopa kutumia sauti zao na ambapo maendeleo yamekwama. Katika njia hii, wajasiriamali wanajizuia kuanzisha biashara mpya kutokana na kanuni kandamizi au zisizotekelezwa kwa usawa. Taasisi za serikali zinaendelea kuwa dhaifu, zenye kugubikwa na rushwa na zisizo na ufanisi. Shule na vituo vya afya havina rasilimali vinavyohitaji na hivyo kushindwa kuwahudumia wahitaji. Vyombo vya usalama vinaogopwa na vinaendeshwa nje ya utawala wa sheria. Watu hawawaamini jirani zao na hawajui wana mtii nani au wapo upande gani. Raia wanaogopa kutoa maoni yao na hivyo kukwaza mijadala ambayo inahitajika sana ili ufumbuzi bora zaidi uweze kufikiwa. Katika mwelekeo huu, jitihada za mamilioni ya Watanzania wenye vipaji na wanaofanya kazi kwa bidii – hususan vijana – hazitaweza kuleta matokeo mazuri inavyostahili.

Ni njia ipi nchi itachukua? Ni wazi njia ipi ingependelewa zaidi, lakini si wakati wote ni rahisi kuchukua njia hiyo. Inahitaji jitihada kubwa, subira na hata ujasiri. Uzuri ni kwamba tayari Watanzania wana amali zitakazoweza kuwasaidia sana – moyo wa ushirikiano, majadiliano na mshikamano kama jamii – mambo ambayo yamekita mizizi sana hapa. Nimeshuhudia moyo huu kila siku kwa miaka yote minne niliyokuwa hapa nchini. Kuzishikilia na kujenga katika amali hizi kutainufaisha nchi hii kwa miaka mingi ijayo. Ninapoondoka Tanzania mwezi huu, ninakumbuka yale aliyosema Mwalimu Nyerere pale alipokutana na Rais Kennedy katika Ikulu ya White House mwaka 1963 – “tukiwa na marafiki duniani, katika pande zote za dunia, tuna uhakika wa kushinda.” Kwa hakika, yatupasa kushikana mikono na kuchukua njia hii pamoja.

 

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Ofisi ya Habari ya Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam kwa simu namba: +255 22 229-4000 au kwa barua pepe: DPO@state.gov.