Flag

An official website of the United States government

Tanzania kuwa Nchi Lengwa kwa Mpango wa Serikali ya Marekani wa Kupata Chanjo Duniani
(Global VAX) Unaolenga Kuongeza Chanjo ya UVIKO-19
4 MINUTE READ
Machi 3, 2022

Global VAX itatoa rasilimali za ziada kusaidia mpango wa kitaifa wa chanjo wa Tanzania

Serikali ya Marekani kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) litaongeza rasilimali kwa Tanzania kupitia mpango wake wa upatikanaji wa chanjo duniani au Global VAX, hizi ni juhudi za serikali ya Marekani kuhakikisha chanjo zinatoka kwenye chupa na kuchomwa kwenye mikono. Msimamizi wa Shirika la USAID Bi. Samantha Power alieleza kuchaguliwa kwa Tanzania katika mpango huu wa chanjo duniani leo alipokuwa anazungumza na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Kama sehemu ya juhudi hizi, Shirika la USAID linapanga kuratibu nyongeza ya Dola za Marekani milioni 25 nchini Tanzania. Ufadhili huu utasaidia shughuli za kuongeza viwango vya chanjo, ikiwa ni pamoja na kushughulikia imani na mahitaji ya chanjo na kuongeza ufikiaji wa maeneo ya chanjo. Afua zote zinaratibiwa kwa karibu na Serikali ya Tanzania, kulingana na mipango iliyopo ya chanjo nchini Tanzania, na itasaidia watu kupata chanjo kwa haraka na usawa. Usaidizi huu wa ziada unatokana na zaidi ya dola za Marekani milioni 42.1 ambazo Shirika la USAID, Kituo cha Kudhibiti Magonjwa nchini Marekani, Idara ya Ulinzi ya Marekani, na Shirika la kujitolea la Marekani wametoa nchini Tanzania kukabiliana na UVIKO-19. Uwekezaji huu umesaidia kuzuia, kutibu, na kufuatilia ugonjwa huo.

Global VAX ni juhudi ya Serikali ya Marekani kusaidia kufikia lengo la kimataifa la kuchanja asilimia 70 ya watu duniani dhidi ya UVIKO-19 mwaka wa 2022. Global VAX itahimiza usaidizi na rasilimali ili kuongeza ufikiaji wa chanjo za UVIKO-19 katika kundi la awali la nchi za Afrika kusini mwa jangwa la sahara, ikiwemo Tanzania. Global VAX imejengwa juu ya dhamira ya Rais Biden ya kuchangia zaidi ya dozi bilioni 1.2 za chanjo ulimwenguni kote kufikia mwisho wa 2022 na inazidisha juhudi za kupata chanjo kwenye mikono. Akiwa mfadhili mkubwa wa chanjo nchini Tanzania, Serikali ya Marekani imetoa karibu chanjo milioni 5, na dozi za ziada zitatolewa katika miezi ijayo.

Mpaka Februari 24, 2022, asilimia saba ya Watanzania wanaostahili wamepatiwa chanjo kamili. Uwekezaji huu mpya unalenga kuongeza kasi ya viwango vya chanjo, kusaidia Serikali ya Tanzania kufikia lengo lake la asilimia 60 ya watu wanaostahiki kupata chanjo ifikapo mwisho wa Juni 2022.

Global VAX itaongeza usaidizi na kuimarisha uratibu wa kimataifa ili kutambua na kushinda kwa haraka vikwazo vya upatikanaji wa chanjo. Kufikia sasa, Marekani tayari imetoa dola bilioni 1.7 kusaidia kazi ya utayari wa chanjo.

Katika wito huo, Balozi wa Marekani nchini, Donald Wright aliangazia uwekezaji huu kama kielelezo zaidi cha ushirikiano wa muda mrefu wa Serikali ya Marekani na Tanzania. Alisema, “Ongezeko hili la fedha mpya linawezekana nchini Tanzania kwa sababu linatokana na uwekezaji wetu wa miongo kadhaa katika sekta ya afya, kwa kutumia ushirikiano na miundo yetu iliyopo kuwafikia Watanzania kwa haraka na chanjo.”

Rasilimali za ziada kutoka Global VAX zitawekezwa kimkakati ili kuendana na juhudi zinazoendelea za Tanzania na kusaidia kuharakisha mpango wa taifa wa chanjo ya UVIKO-19. USAID na washirika wake watafanya kazi na Tanzania kuimarisha mifumo ya afya na kusaidia kuongeza upatikanaji wa chanjo miongoni mwa watu walio hatarini na ambao ni vigumu kuwafikia.