Tanzania na Marekani Zasherehekea Usambazaji wa Vitabu vya Sekondari Milioni 2.5 Nchini Kote Tanzania

U.S. Ambassador Mark Childress and President Jakaya Kikwete pose with science textbooks donated by the U.S. Government
Balozi wa Marekani nchini Mark B. Childress na Rais Jakaya Kikwete wakati wa makabidhiano ya vitabu vya sayansi vilivyotolewa na serikali ya Marekani. (Picha kwa hisani ya Ubalozi wa Marekani)
Balozi wa Marekani nchini Mark B. Childress na Rais Jakaya Kikwete wakati wa makabidhiano ya vitabu vya sayansi vilivyotolewa na serikali ya Marekani. (Picha kwa hisani ya Ubalozi wa Marekani)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete  na Balozi wa Marekani nchini Mark B. Childress  hapo jana walishiriki katika hafla ya kukabidhi rasmi vitabu vya shule za sekondari vipatavyo  milioni 2.5 kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi. Rais Kikwete alitoa ombi la vitabu hivyo kwa Rais Barack Obama wakati wa ziara yake nchini Tanzania hapo Juni 2013. Vitabu hivyo vimetolewa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).  Tayari vitabu vyote milioni 2.5 vya masomo ya hisabati, fizikia, kemia na baiolojia vya kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, vimeshasambazwa katika shule za sekondari Tanzania bara. Usambazaji huo ulifanywa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania mwezi Januari 2015.

Hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Mtakuja, Kunduchi jijini Dar es Salaam ilihudhuriwa pia na wawakilishi wa wizara ya Elimu, Ofisi ya Waziri Mkuu na umati wa zaidi ya watu 4,000 ukijumuisha wanafunzi, viongozi wa kiserikali na walimu kutoka pande zote za jiji la Dar es Salaam.

Katika hotuba yake aliyoianza kwa kutumia lugha ya Kiswahili, Balozi Childress alisema “Ili kujifunza, lazima msome. Na vitabu kama hivi ni ufunguo wa maendeleo ya siku zijazo – elimu ya sayansi na teknolojia ni msingi wa ustawi wa kiuchumi.” Aliendelea kusema kuwa “ Tumetembelea baadhi ya madarasa ya shule hii, na tumefurahishwa sana kuona jinsi wanafunzi hawa wanavyojifunza.  Ninakuhakikishia Mheshimiwa Rais kwamba  – miongoni mwa wanafunzi tuliowaona darasani hivi leo watapatikana wanasayansi mahiri. Hii ni kwa sababu hivi leo Rais Kikwete amewatembelea darasani kwao wakiwa na vitabu vyao vipya. Hili ni jambo zuri sana na la kipekee.”

Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete, Rais Jakaya Kikwete na Balozi wa Marekani nchini Mark B. Childress wakiwa pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mtakuja katika hafla ya makabidhiano ya vitabu vya sayansi. (Picha kwa hisani ya Ubalozi wa Marekani)
Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete, Rais Jakaya Kikwete na Balozi wa Marekani nchini Mark B. Childress wakiwa pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mtakuja katika hafla ya makabidhiano ya vitabu vya sayansi. (Picha kwa hisani ya Ubalozi wa Marekani)

Serikali za Tanzania na Marekani zinachukua jitihada za pamoja katika kuweka msingi imara wa stadi mbalimbali kwa kutoa elimu bora, sio tu katika masomo ya sayansi, bali pia katika kuandika, kusoma na kuhesabu.  Kusaidia programu mbalimbali zinazolenga kuongeza upatikanaji wa elimu katika nchi zinazoendelea – hususan programu zinazolenga kuongeza fursa za elimu kwa wasichana  kumethibitika kuleta mafanikio makubwa na endelevu ya kiuchumi. Katika utafiti uliofanyika katika nchi 100, Benki ya Dunia imebaini kuwa ongezeko la asilimia moja ya idadi ya wanawake wanaopata elimu ya sekondari huongeza pato la jumla la taifa kwa asilimia 0.3. Hali kadhalika, tafiti nyingine mbalimbali zimebaini kuwa wanawake wenye elimu huwekeza hadi asilimia 90 ya mapato yao katika familia zao.

Kukabidhiwa kwa vitabu hivi kunafuatia mradi mwingine kama huu uliofadhiliwa na USAID hapo mwaka 2008, ambapo kwa kupitia ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha South Carolina na Wizara ya Elimu ya Zanzibar, zaidi ya vitabu milioni moja na zana nyingine za kujifunzia ziliandaliwa na kusambazwa visiwani kote Zanzibar.

Mbali na kusaidia utayarishaji na uchapishaji wa vitabu, programu za elimu za USAID nchini Tanzania zimekuwa pia zikilenga katika kuinua stadi za kusoma.  Programu hizo ni pamoja na ile ya kuandaa na kusambaza zana za kufundishia, utoaji mafunzo kwa walimu na kuwapatia wazazi na wanajamii nyenzo za kuwasaidia watoto kujifunza kusoma.