Flag

An official website of the United States government

Serikali ya Marekani inaadhimisha miaka mitano ya kuboresha huduma za VVU/UKIMWI,
Kifua Kikuu na uzazi wa mpango kupitia miradi ya USAID Boresha Afya.
3 MINUTE READ
Novemba 11, 2021

Dodoma – (Novemba 11, 2021) wawakilishi wa serikali ya Marekani na serikali ya Tanzania wamesherehekea mafanikio ya miradi ya Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Boresha Afya Kanda ya Kaskazini-Kati na Kusini. Kupitia ushirikiano imara na wa muda mrefu na serikali ya Tanzania, miradi ya Boresha afya yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 222, iliboresha afya za mamilioni ya Watanzania katika mikoa 12 nchini kote.

VVU, malaria, na kifua kikuu ni miongoni mwa sababu kuu za maradhi, ulemavu na vifo nchini Tanzania. Kukosekana kwa huduma za afya ya mama na mtoto na uzazi wa mpango kwa raia wa Tanzania, hususan kwa wanawake na vijana pia kunachangia afya duni. Watanzania wengi hawawezi kupata huduma bora na jumuishi za afya huku uratibu dhaifu kati ya vituo vya kutolea huduma za afya na jamii ukisababisha kutokuwepo kwa msaada wa kutosha kwa wagonjwa.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, miradi ya Boresha Afya ilitumia njia madhubuti na za kibunifu kushughulikia changamoto hizi. Malengo makuu ya miradi hii yalikuwa ni kuongeza upatikanaji- na kuboresha huduma za afya katika ngazi ya jamii. Ili kufikia malengo yake, miradi iliunganisha huduma za VVU/UKIMWI na zile za afya ya uzazi, kifua kikuu na uzazi wa mpango na kuweka uratibu kati ya watoa huduma za afya na jamii.

Kutokana na miradi ya Boresha Afya, zaidi ya Watanzania milioni 8.3 walipata huduma za kupima VVU ambapo karibu watu laki 3.4 waligundulika kuwa wanaishi na VVU. Wote walianzishiwa matibabu ya kuokoa maisha kwa kutumia dawa za kufubaza VVU. Zaidi ya hayo, Boresha Afya iliwafikia zaidi ya wanufaika milioni 10 kupitia utoaji wa huduma za uzazi wa mpango.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkazi wa USAID V. Kate Somvongsiri alimueleza mgeni rasmi, Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu kuwa; “Mheshimiwa Waziri, tunatarajia mafanikio yaliyoainishwa katika mkutano huu yataihimiza wizara yako kuweka mazingira wezeshi yatakayoendelea kusaidia mfumo shirikishi wa utoaji wa huduma za afya kwa Watanzania wote ili mafanikio haya yaweze kuwa endelevu.