Flag

An official website of the United States government

Marekani Yaipatia Tanzania Zaidi ya Dozi Milioni Moja ya Chanjo ya Johnson & Johnson
4 MINUTE READ
Julai 24, 2021

Dar es Salaam, TANZANIA.

Ubalozi wa Marekani Jijini Dar es Salaam, Tanzania unatangaza kuwa Marekani imetoa msaada wa zaidi ya dozi milioni moja za chanjo dhidi ya COVID-19 aina ya Johnson & Johnson, kama sehemu ya jitihada za kimataifa katika kukabiliana na janga la COVID-19. Msaada huu ni sehemu ya ahadi ya Marekani ya kuanza kutoa angalau dozi milioni 25 kwa Afrika kati ya dozi milioni 80 zilizoahidiwa kwa bara hili.  Serikali ya Marekani inaendesha shughuli hii kwa uratibu wa karibu na Umoja wa Afrika na Kituo cha Afrika cha Kudhibiti Maradhi (Africa CDC) hususan kuhusu mgao wa chanjo kwa kila nchi.  Dozi hizi za chanjo ziliwasili Jijini Dar es Salaam tarehe 24 Julai kupitia mpango wa usambazaji chanjo kimataifa wa COVAX.

Msaada huu utasaidia kuwalinda watu wa Tanzania dhidi ya athari za janga la COVID-19 na kuanza kupunguza vikwazo katika jitihada za kuujenga upya uchumi wa Tanzania.

“Tunachangia chanjo hizi ili kuokoa maisha na kuiongoza dunia katika kulitokomeza janga hili. Aidha, kuchangia kwetu chanjo hizi ni kielelezo cha uimara wa ubia wetu wa miaka 60 na dhamira yetu ya dhati kwa Tanzania,” alisema Balozi Wright.

Dozi hizi zaidi ya milioni moja ni sehemu ya ahadi ya utawala wa serikali ya Marekani kuchangia na dunia mgao wake wa chanjo. Wakati tukipambana na COVID-19 nyumbani na tukipambana kulitokomeza janga  hili duniani kote, Rais Biden ameahidi kuwa Marekani itakuwa ghala la silaha ya chanjo kwa dunia.

Kama Rais Biden alivyosema,

“Toka mwanzo wa Urais wangu, tumeweka bayana kuwa tunahitaji pia kupambana na virusi hivi katika ngazi ya kimataifa.  Hii ni kuhusu wajibu wetu – dhima yetu ya kibinaadamu ya kuokoa maisha ya watu wengi kwa kadri inavyowezekana – na wajibu wetu kwa maadili yetu.  Tutasaidia kuiongoza dunia kutokomeza janga hili, tukifanya kazi bega kwa bega na wabia wetu duniani kote.”