Flag

An official website of the United States government

Ushirikiano wa Marekani nchini Tanzania na duniani kote katika mapambano dhidi ya COVID -19
5 MINUTE READ
Aprili 21, 2020

Dk. Inmi K. Patterson, Kaimu Balozi wa Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania 

April 20, 2020

Simulizi za uongozi wa Marekani kwenye mapambano ya dunia dhidi ya Covid -19 ni simulizi za siku kadhaa, miezi na miongo. Kila siku msaada mpya wa kiufundi na vifaa unaotolewa na Marekani huwasili kwenye hospitali na maabara duniani kote. Jitihada hizi zinajenga msingi wa miaka mingi wa utaalamu, ukarimu na mipango isiyo na mfano katika historia.

Serikali ya Marekani inafanya kazi bega kwa bega na marafiki na washirika wetu duniani kote kuhakikisha usalama wa afya duniani. Msaada wetu ni zaidi ya fedha na mahitaji. Ni wataalam wetu walioko duniani kote na wale wanaoendelea kutoa mafunzo hadi leo kupitia mikutano ya kimtandao. Ni madaktari na wataalamu wa afya ya jamii, waliopata mafunzo, shukurani ziende kwa ufadhili wa Marekani na taasisi zake za kielimu. Ni mifumo ya ugawaji tulioiweka wazi na inayoendelea kwa ajili ya uzalishaji na usambazaji wa mahitaji ya dawa zinazohitajika sana, zenye ubora wa hali ya juu duniani kote.

Marekani inatoa misaada ya maendeleo kwa ajili ya kuimarisha mahusiano na mataifa mengine duniani kote kwasababu tunaamini ni jambo lililo sahihi kufanya. Tunafanya hivyo pia kwasababu majanga yanapotokea hayaheshimu mipaka ya nchi. Tukiweza kuzisaidia nchi kudhibiti milipuko ya magonjwa, tutaokoa maisha ya watu ughaibuni na nyumbani Marekani.

Hapa nchini Tanzania, dhamira yetu ya pamoja kuhusu usalama wa afya haijawahi kuwa ya wazi na muhimu zaidi kuliko ilivyo sasa. Wataalamu wa maabara na wa afya ya jamii waliopata mafunzo kutoka Marekani, wanawapima washukiwa wa ugonjwa, wanawafuatilia waliokutana nao, wanabuni mikakati ya kujenga uelewa kwa wananchi na jitihada za mawasiliano hatarishi. Wataalam wa Marekani kutoka Taasisi ya Kimarekani ya Udhibiti wa Magonjwa (CDC), Shirika la Misaada na Maendeleo la Marekani (USAID) na Wizara ya Ulinzi, wanashauriana na wenzao wa Tanzania, kushughulikia msaada wa afya uliopo, na kuhakikisha kuna mwendelezo wa uhusiano huo, utakaojenga na kusaidia mfumo wa afya nchini Tanzania.

Uwepo wa pamoja wa ofisi za Taasisi ya Marekani ya Udhibiti wa Magonjwa (CDC) ndani ya Wizara ya Afya ni ukumbusho mzuri kwamba ushirikiano wetu kwenye masuala ya afya uko kwenye kitovu cha uhusiano na Tanzania na watu wake. Dhamira ya Marekani kwenye ushirikiano huo bado iko imara, iliyojengwa kutokana na uwekezaji wa karibu shilingi trilioni 17.4 katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, zikiwemo zaidi ya shilingi 200,000/= kwa kila mtanzania aliye hai leo, katika kuunga mkono sekta ya afya nchini Tanzania. Mwaka huu peke yake, msaada wa walipa kodi wa Marekani utatoa karibu shilingi trilioni 1.2 kwa ajili ya kushughulikia VVU/UKIMWI, ikiwemo karibu shilingi bilioni 275 kwa ajili ya tiba ya kuokoa maisha ya dawa za kufubaza virusi vya ukimwi na bidhaa zingine za afya, wakati pia ikitoa ufadhili kwa ajili ya mishahara kwa baadhi ya wafanyakazi muhimu ambao ni nguvukazi ya Wizara ya Afya nchini kote.

Wakati uwekezaji wetu nchini Tanzania ni wa kiwango kikubwa na wa kudumu ni sehemu moja tu ya uwekezaji wa dola za Marekani bilioni 100 ambapo Marekani imefanya kwa ajili ya afya ya waafrika barani kote katika kipindi cha miongo miwili iliyopita. Katika kukabiliana na mlipuko wa COVID -19, dhamira ya Marekani kwa Marekani, kwa Africa na kwa afya ya dunia haijawahi na haitatetereka. Tangu mlipuko wa COVID -19 serikali ya Marekani imetoa msaada wa dola za Marekani milioni 500 hadi sasa duniani kote, zikiwemo shilingi bilioni 3.2 kwa ajili ya kusaidia juhudi za Tanzania.

Marekani inafadhili karibu asilimia 40 ya programu za misaada ya afya duniani, kufikia hadi uwekezaji wa dola za Marekani bilioni 140 katika kipindi cha miaka 20 iliyopita – ambapo ni mara tano zaidi ya mfadhili anayefuatia. Tangu 2009, walipa kodi wa Marekani kwa ukarimu wamefadhili zaidi ya dola za Marekani bilioni 100 kwenye misaada ya afya na karibu dola za Marekani bilioni 70 kwenye misaada ya kibinadamu duniani. Fedha hizi zimeokoa maisha, zimewalinda watu walio katika mazingira hatarishi ya magonjwa, zimejenga taasisi za afya, ikiwemo wale walio mstari wa mbele wa mapambano dhidi ya COVID -19, na zimeimarisha amani za jamii na mataifa.

Hakuna nchi itakayopambana na COVID -19 peke yake. Kama tulivyofanya mara kadhaa, Marekani itawasaidia wengine kwenye nyakati zao za uhitaji mkubwa. Tutaendelea kuzisaidia nchi mbalimbali kujenga mifumo imara ya afya inayoweza kuzuia, kugundua, na kukabiliana na milipuko ya magonjwa ya kuambukiza. Kwa pamoja tunaweza kuishinda changamoto hii ya kihistoria iliyoletwa na janga la COVID -19, kila siku, duniani kote.