Flag

An official website of the United States government

Dhamira ya dhati ya Marekani na ubia wake usioyumba na Tanzania
7 MINUTE READ
Agosti 5, 2020

Kwa mara ya kwanza nilitembelea Tanzania zaidi ya miaka 30 iliyopita nilipofanya kazi kama daktari wa kujitolea katika hospitali ya umma huko Zanzibar. Katika kipindi hicho cha majira ya kiangazi ninachokikumbuka sana, niliwatibu watoto waliokuwa wakiugua utapiamlo, malaria, minyoo na kifua kikuu. Lakini pia nilivutiwa mno na watu wa Tanzania; walikuwa wema, wakarimu na wakiwachukulia wageni kama sehemu ya familia zao. Katika miaka iliyofuata, nilifanya kazi kama daktari katika jimbo la Texas na baadaye niliajiriwa kama mtumishi wa umma jijini Washington, ambapo hatimaye niliongoza Idara ya Udhibiti Maradhi na Kukuza Afya kwa takriban miaka minane. Sikuwahi kuota kwamba maisha yatanirejesha pale nilipoanzia maisha yangu ya kikazi. Leo hii, ni heshima kubwa kwangu kuiwakilisha nchi yangu kama Balozi wa Marekani nchini Tanzania. Uzoefu wangu nikiwa kijana mdogo huko Zanzibar ulikuwa na matokeo na mchango mkubwa katika maisha yangu. Hivi sasa ninaporejea kama Balozi wa Marekani, nimedhamiria kwa dhati kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya watu wa Tanzania na watu wa Marekani ili kuleta amani na ustawi zaidi kwa nchi zetu mbili.

Kwa msingi na moyo huo, ninakusudia kuinua zama mpya ya ushirikiano na mahusiano baina ya nchi zetu mbili na ubia utakaowagusa moja kwa moja watu wa Tanzania. Ninatarajia kutembelea majiji, miji na vijiji mbalimbali vya Tanzania, kuanzia Kagera hadi Mtwara na kutoka Kigoma hadi visiwa vya Zanzibar. Nitapenda kusikia kutoka wanachama wa jumuiya za wafanyabiashara wa Kitanzania na Kimarekani, vyuo vikuu na taasisi mbalimbali kuhusu mawazo na maoni yao kuhusu namna tunavyoweza kupanua jitihada zetu na kubuni njia mpya za ushirikiano zitakazotuwezesha kujenga kizazi kipya cha viongozi na kujenga mustakabali mwema kwa Watanzania wote. Toka kuapishwa kwangu, nimekuwa na mikutano mingi ya mashauriano na taasisi mbalimbali za Serikali ya Marekani, taasisi za ushirikiano baina ya nchi zetu na asasi za kiraia jijini Washington DC. Katika kila mmoja kati ya mikutano hiyo, jambo kuu lililojitokeza ni ari kubwa, hamasa na msaada kwa mustakabali mwema wa Tanzania na kwa uhusiano rasmi baina ya nchi zetu. Nikiwa balozi, vipaumbele vyangu vikuu vitakuwa ni kuboresha afya, kuongeza kasi ya ukuaji uchumi na kukuza uwekezaji kwa vijana. Aidha, kuhakikisha usalama wa raia wa Marekani na taifa la Marekani pamoja na wafanyakazi wa Ubalozi wa Marekani ni kipaumbele cha juu kabisa.

Kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20 iliyopita, Marekani imetoa zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 7.5 kama msaada rasmi kwa Tanzania, huku takriban Dola za Kimarekani bilioni 4.9 kati ya fedha hizo, zikielekezwa katika kuboresha afya ya Watanzania. Nikiwa daktari, naelewa umuhimu wa jitihada hizi. Nimedhamiria kwa dhati kuhakikisha kuwa ubia wa Marekani unaendelea kuwa imara. Mwaka huu pekee, walipa kodi wa Marekani watatoa Dola za Kimarekani milioni 5.6 kusaidia mapambano dhidi ya COVID-19 nchini Tanzania. Hii ni sawa na Shilingi bilioni 12.9.

Mazingira ya kibiashara ya Tanzania yenye changamoto nyingi, yanatoa hali ya tumaini lakini pia yanaweza kuwafanya watu kusitasita. Kuna tumaini kwa sababu, kama sote tujuavyo, Tanzania ni nchi yenye fursa zisizomithilika. Wakati huo huo, kuna hali ya kusitasita miongoni mwa wawekezaji kwa sababu ya mabadiliko ya kisera yasiyo na uwazi na yasiyotabirika; sheria za mikataba zinazobadilika badilika, matumizi ya mbinu zisizo rafiki za ukusanyaji mapato; nishati isiyoaminika na yenye gharama kubwa; miundombinu hafifu; na vikwazo katika upatikanaji na utumiaji wa ardhi.

Ni lazima sekta ya umma na sekta binafsi zishirikiane na kujenga hali ya kuaminiana iwapo kweli tunataka ukuaji wa uchumi wenye wigo mpana, ulio jumuishi na endelevu.  Kwa kuongeza uwekezaji wa sekta binafsi, Tanzania inaweza kutatua mahitaji yake muhimu ya miundombinu kama vile upatikanaji wa nishati ya gharama nafuu kwa wote na mitandao ya usafirishaji wa umma wakati huo huo ikijenga uwezo wa rasilimali watu inayohitajika kuendeleza zaidi hatua iliyofikiwa hivi karibuni ya kuingia katika kundi la nchi za uchumi wa kati na hatimaye kuwatoa watu wengi zaidi katika umasikini.

Biashara za Wamarekani zimekuwa mfano duniani kote kwa kufuata taratibu za kiuendeshaji zisizogubikwa na rushwa, kuzingatia sheria na miongozo ya nchi husika pamoja na kutekeleza wajibu wa kampuni kwa jamii ikiwemo kurejesha sehemu ya faida yake kwa jamii inayozunguka (corporate social responsibility). Nina ari kubwa ya kufanya kazi na Serikali ya Tanzania kuimarisha ushirikiano kati ya makampuni ya Kimarekani na Tanzania wakati tukiendelea kutafuta fursa zaidi na kupanua masoko kwa faida yetu sote. Kwa kupanua ubia wetu wa kibiashara na kufanya kazi pamoja, tunaweza kuzifanya Marekani na Tanzania kuwa wabia wa ngazi na kiwango cha juu kabisa wa biashara na uwekezaji.

Mojawapo ya injini zinazoiendesha Tanzania ni vijana wake. Nina amini kwa dhati kabisa katika nafasi ambayo vijana wanaweza kuichukua, na ni lazima waichukue, katika kujenga taifa la baadaye lenye ustawi zaidi. Kupitia programu zetu mbalimbali za mabadilishano ya kikazi, kitamaduni na kielimu pamoja na miradi ya kuleta mabadiliko inayoendeshwa na washiriki wa programu hizo katika jamii zao pindi warejeapo Tanzania, Marekani inaendelea kujengea uwezo kizazi kijacho cha viongozi wa Tanzania wa asasi za kiraia, serikali na biashara.

Kuzingatia utawala wa sheria na kuimarisha taasisi za kidemokrasia ndio msingi wa kufanikiwa kwa jitihada hizi zote zilizoelezwa. Katiba zetu mbili zinatambua nafasi na umuhimu wa kipekee wa demokrasia ya raia pale zinapoanza kwa kutamka: “We the People,” “Sisi Wananchi.” Hii ni mojawapo ya amali za msingi tunazochagia na zinazounganisha nchi zetu. Hata hivyo, hali ya kuendelea kuminywa kwa demokrasia na kumomonyoka kwa misingi na kanuni za demokrasia kumekwaza haki za msingi na uhuru binafsi wa raia wa Tanzania, mathalan, uhuru wa kujieleza na kujumuika. Nina dhamira ya dhati ya kufanya kazi na Serikali, Balozi nyingine zenye maono kama yetu, Asasi za Kiraia na Taasisi za Kimataifa ili kubadilisha mwelekeo huu unaotia shaka. Ninatarajia kutekelezwa kwa vitendo hakikisho lililotolewa na Rais Magufuli tarehe 21 Januari kwamba uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020 utakuwa huru, wa haki na wenye uwazi pamoja na mwaliko alioutoa kwa waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa. Tunatarajia uchaguzi ambao raia na wagombea wote kutoka vyama vyote wataweza kukusanyika kwa amani, kueleza maoni yao na kufanya kampeni zao kwa usawa.

Huu ni wakati mzuri na fursa ya kipekee – hii ni awamu mpya katika ushirikiano wetu ambayo nina fahari kuiongoza. Napenda kurejea maneno ya Rais wa sita wa Marekani John Adams, pale alipoteuliwa kuwa balozi wetu wa kwanza nchini Uingereza. Bila kunukuu neno kwa neno alilotamka, alisema: Nitajihesabu kuwa mtu mwenye furaha zaidi duniani, pale nitakapoweza kuwa nyenzo ya kurejesha imani, hali ya kuaminiana na upendo baina ya mataifa yetu. Siwezi kufikiria lengo lililo kubwa zaidi ya hilo au heshima kubwa zaidi ya hiyo. Kwa kufanya kazi pamoja Marekani na Tanzania tunaweza kuimarisha uchumi wetu, kuwafanya raia wetu kuishi maisha yenye afya zaidi na kuwajenga viongozi wetu wa kesho. Kwa Pamoja TutasongaMbele!