Wafanyakazi wa Kujitolea wa Kimarekani 36 Kutoa Elimu ya Afya na Kuimarisha Kilimo Endelevu katika Wilaya 16

Wafanyakazi wa Kujitolea wa Kimarekani 36 Kutoa Elimu ya Afya na Kuimarisha Kilimo Endelevu katika Wilaya 16. (Picha: Ubalozi wa Marekani)
Wafanyakazi wa Kujitolea wa Kimarekani 36 Kutoa Elimu ya Afya na Kuimarisha Kilimo Endelevu katika Wilaya 16. (Picha: Ubalozi wa Marekani)
Wafanyakazi wa Kujitolea wa Kimarekani 36 Kutoa Elimu ya Afya na Kuimarisha Kilimo Endelevu katika Wilaya 16. (Picha: Ubalozi wa Marekani)

Dar es Salaam, TANZANIA. Tarehe 22 Aprili, Balozi wa Marekani nchini Tanzania Mark Childress aliwaapisha wafanyakazi wa kujitolea wa Peace Corps wapatao 36 ili kuanza utumishi wao wa miaka miwili nchini Tanzania. Wafanyakazi hawa wa kujitolea watahudumu katika wilaya 16 nchini kote Tanzania wakitoa elimu ya afya na mbinu mbalimbali za kilimo endelevu katika jamii watakazokuwa wakiishi. Hafla ya kuapishwa kwa wafanyakazi hao ilifanyika katika Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Bi Regina Kikuli, Mkurugenzi wa Peace Corps nchini Dk. Elizabeth O’Malley pamoja na waliowahi kuwa wafanyakazi wa kujitolea wa Peace Corps sehemu mbalimbali duniani. Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na maafisa kutoka idara mbalimbali za serikali na taasisi zinazojihusisha na wafanyakazi wa kujitolea.

Wafanyakazi wa kujitolea walioapishwa leo, watapangiwa kufanyakazi katika wilaya za Iringa, Mufindi, Kondoa, Mbinga, Masasi, Ludewa, Lushoto, Songea na Kiteto. Wengine watapangiwa katika wilaya za Makete, Singida vijijini, Same, Njombe, Kilolo na Makambako.

amb_earthday2015_600pxHuko watatoa msaada wa mafunzo kuhusu elimu ya mazingira ikiwa ni pamoja na masuala yanayohusu uhifadhi wa ardhi, utunzaji wa vyanzo vya maji na mbinu za kilimo na utunzaji wa misitu (agro- forestry), wakiweka msisitizo katika kufanya kazi kwa ubia na wanawake na vijana. Pia watatoa mafunzo na kuwezesha kuanzishwa kwa kilimo hai cha bustani (bio-intensive gardens) ili kuongeza upatikanaji wa chakula, na kuboresha lishe ya kaya pamoja na shughuli nyingine za kujiongezea kipato.

Vile vile wafanyakazi hawa wa kujitolea watasaidia katika kuimarisha afya ya jamii kwa kufanya kazi na vijana, watoa huduma za afya na vikundi vya kijamii ili kukuza tabia zitakazowawezesha kulinda afya zao, ikiwa ni pamoja kujilinda dhidi ya VVU/UKIMWI, kutoa  matunzo na huduma nyingine kwa watu wanaoishi na VVU, yatima na watoto walio katika mazingira magumu na hatarishi. Wafanyakazi wa kujitolea hufanya kazi kwa karibu na kamati za afya za vijiji ili kuchambua mahitaji ya jamii na mambo ya kupewa kipaumbele.

Peace Corps ni taasisi ya Serikali ya Marekani iliyoanzishwa na Rais John F. Kennedy mwaka 1961 ambayo hivi sasa inahudumia zaidi ya wafanyakazi wa kujitolea zaidi ya 8,000 katika zaidi ya nchi 75 duniani. Kwa miaka 48, Peace Corps imekuwa taasisi inayoendesha shughuli za mabadilishano ya kiufundi na kitamaduni zisizoegemea mrengo wowote wa kisiasa na kidini. Peace Corps ina dhamira ya kukuza amani na urafiki duniani kwa kutekeleza malengo matatu yafuatayo:

  • Kutoa wafanyakazi wa kujitolea wa Kimarekani watakaochangia kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika nchi itakayohitaji wafanyakazi hao;

 

  • Kukuza uelewa kuhusu Wamarekani miongoni mwa watu katika jamii zinazohudumiwa na Wafanyakazi wa kujitolea;

 

  • Kuimarisha uelewa wa Wamarekani kuhusu dunia na watu wake.

Zaidi ya Wafanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corps wapatao 2,000 wamehudumu nchini Tanzania toka mwaka 1962. Peace Corps hutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa kujitolea wa Marekani wanao fanyakazi katika jamii katika Nyanja za elimu ya sekondari (wakifundisha hisabati, sayansi na teknolojia ya mawasilianoa), afya na elimu ya mazingira.

Kwa taarifa Zaidi, tafadhali wasiliana na Japhet Sanga (SangaJJ@state.gov), Afisa Habari Mwandamizi wa Ubalozi wa Marekani