Wizara ya Fedha ya Marekani Yamuwekea Vikwazo Kinara wa Kitanzania wa Usafirishaji dawa za kulevya na Mtandao wake Katika Nchi za Afrika Mashariki

Hatua hii inaulenga Mtandao wa Usafirishaji Dawa za Kulevya wa Hassan, mtandao unaohusika katika usafirishaji wa Cocaine na Heroin

WASHINGTON – Leo hii, Idara ya Kudhibiti Mali Haramu za Raia wa Kigeni (OFAC) ya Wizara ya Fedha ya Marekani imemtambua na kumuorodhesha raia wa Tanzania Ali Khatib Haji Hassan (ambaye pia anajulikana kama “Shkuba”) kama gwiji au kinara wa usafirishaji wa dawa za kulevya (drug kingpin) na kuutambua mtandao wake  kama kikundi kilichohusika na usafirishaji mkubwa sana wa kimataifa wa dawa hizo chini ya Sheria ya Marekani ya Kuwadhibiti Wafanyabiashara Wakubwa wa Dawa za Kulevya  (U.S. Kingpin Act). Hassan ni gwiji wa biashara ya kimataifa ya dawa za kulevya ambaye kwa kupitia mtandao wake wenye makao yake katika nchi za Afrika Mashariki, amehusika na usafirishaji wa tani nyingi za dawa za kulevya aina ya heroin na cocaine katika mabara ya Afrika, Ulaya, Asia na Amerika ya Kaskazini. Kufuatia hatua hiyo ya leo, mali zote zinazomilikiwa na Hassan pamoja na mtandao wake zilizopo nchini Marekani, au zilizo chini ya usimamizi wa raia wa Marekani zinazuiliwa. Hali kadhalika, raia wote wa Marekani wanapigwa marufuku kufanya biashara ya aina yoyote ile na Hassan na mtandao wake.

Baada ya msako Mkali wa miaka miwili, Hassan alikamatwa na mamlaka za Tanzania hapo mwaka 2014 kwa kuhusika na usafirishaji wa kilogramu 210 za heroin zilizokamatwa Januari 2012 huko Lindi nchini Tanzania. Mara kwa mara Hassan alijaribu kuwahonga maafisa wa serikali katika nchi za Kiafrika ili kukwepa kukamatwa na kushtakiwa kwa kujihusisha kwake na biashara hii haramu.

“Hatua ya leo inalenga kumuwekea vikwazo Ali Khatib Haji Hassan na mtandao wake wa usafirishaji heroin na cocaine duniani kote ili wasiweze kutumia faida itokanayo na biashara yao haramu ikiwa ni pamoja na kuwahonga maafisa wa serikali katika nchi za Kiafrika,” alisema Kaimu Mkurugenzi wa OFAC John E. Smith. “Wasafirishaji wa madawa ya kulevya kama Hassan na mtandao wake ni tishio kubwa kwa mfumo wa fedha wa kimataifa na usalama wa kikanda. Kwa sababu hiyo, Wizara ya Fedha ya Marekani imedhamiria kwa dhati kuwafichua na kuwalenga wale wote wanaojihusisha na kuchochea biashara haramu ya dawa za kulevya duniani.”

Hassan na mtandao wake walipokea tani kadhaa za heroin kutoka vyanzo mbalimbali katika nchi za Kusini-magharibi mwa Asia na tani nyingine nyingi za cocaine kutoka kwa wasambazaji kutoka nchi za Amerika ya Kusini. Toka mwaka 2006 Hassan amekuwa akiwaongoza na kuwezesha wanachama wa mtandao wake kusafirisha shehena za dawa hizo za kulevya kuelekea katika nchi mbalimbali zikiwemo China, nchi za Ulaya na Marekani. Hassan ndiye aliyekuwa msambazaji mkuu kwa wasafirishaji wa dawa hizo waliokuwa Tanzania, mara kwa mara akipokea mamia ya kilo za heroin zilizokuwa zikiingizwa nchini humo kupitia baharini kutoka katika ufukwe wa Makran katika nchi za Pakistan na Iran. Aidha, Hassan alisimamia mtandao mpana katika nchi za Amerika ya Kusini uliokuwa ukisafirisha cocaine kutoka nchi hizo na kuziingiza katika nchi za Afrika Mashariki zikiwa njiani kuelekea Ulaya na China.

Toka mwaka 2000, zaidi ya taasisi na watu 1,800 wameorodheshwa chini ya Sheria ya Marekani ya Kuwadhibiti Wafanyabiashara Wakubwa wa Dawa za Kulevya kama vinara wa biashara hiyo kutokana na ushiriki wao katika usafirishaji wa kimataifa wa dawa za kulevya. Kwa mujibu wa kifungu cha 18 cha Sheria ya Adhabu kwa wanaokiuka sheria hii (Title 18 of the United States Code of Criminal Violation of the Kingpin Act) wale wanaopatikana na hatia chini ya sheria wanaweza kukabiliwa na adhabu ya kulipa fidia ya hadi dola milioni 1.075 kwa kila kosa na hata adhabu nyingine kali zaidi za kijinai. Maafisa wa mashirika na makampuni wanaokiuka sheria hii wanaweza kuhukumiwa kifungo jela cha hadi miaka 30 na faini ya hadi dola milioni 5. Kwa makampuni,faini inaweza kufika dola milioni 10. Aidha, adhabu kwa watu binafsi inaweza kuwa kifungo gerezani cha hadi miaka 10 pamoja na faini.

Kwa ripoti  inayowasilishwa katika Bunge la Congress la Marekani inayomuorodhesha  Ali Khatib Haji Hassan na Mtandao wake kama “vinara wa usafirishaji dawa za kulevya  chini ya Kifungu 805(b)(l) cha Sheria ya Marekani ya Kuwadhibiti Wafanyabiashara Wakubwa wa Dawa za Kulevya, bofya hapa.

Kwa orodha kamili ya watu na taasisi zilizoorodheshwa kama vinara wa usafirishaji wa dawa za kulevya chini ya Sheria ya Marekani ya Kuwadhibiti Wafanyabiashara Wakubwa wa Dawa za Kulevya, bofya hapa.

Kwa taarifa zaidi kuhusu hatua hii ya leo, bofya https://www.treasury.gov/press-center/press-releases/Pages/jl0378.aspx.