Flag

An official website of the United States government

Balozi wa Marekani aainisha uimara wa ushirikiano kati ya Marekani na Tanzania
Katika mhadhara aliotoa katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi
3 MINUTE READ
Febuari 16, 2022

Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dk. Donald Wright leo ametoa mhadhara kuhusu sera ya mambo ya nje ya Marekani na ubia kati ya Marekani na Tanzania kwa wanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi.

Balozi Wright alialikwa kutoa mhadhara huo na Mkuu wa Chuo, Meja Jenerali Ibrahim Mhona.

Katika mada yake, Balozi Wright aliangazia uimara wa ubia wa miaka 60 kati ya Marekani na Tanzania ambao umealeta mafanikio kadha wa kadha kwa nchi zote mbili. Alielezea nguzo kuu za uhusiano kati ya Marekani na Tanzania kuwa ni dhamira ya pamoja ya kuboresha afya na elimu; kuchochea ukuaji wa uchumi na biashara; kuimarisha demokrasia; na kukuza amani na usalama.

“Katika kila eneo kati ya haya, ubia wetu umekuwa na matokeo chanya “Ubia wetu una matokeo chanya katika maisha ya Watanzania wa kawaida wakati tukiendelea kuimarisha zaidi uhusiano baina ya nchi zetu,” alisema.

Akizungumzia masuala muhimu katika ushirikiano wa kiusalama, Balozi Wright alisisitizia jukumu muhimu ambalo Tanzania imekuwa ikilitekeleza katika kusaidia kuhakikisha amani na usalama katika kanda.

“Tanzania ni mbia muhimu katika kukuza amani na utulivu wa kikanda katika ukanda wa Afrika Mashariki,” alisema.

Mara kwa mara Chuo cha Taifa cha Ulinzi huwakaribisha wanadiplomasia kutoa mihadhara kwa wanafunzi wake katika kozi yake ya Ulinzi na Mafunzo ya Kimkakati kama sehemu ya lengo lake la kuwapa watengeneza sera za serikali na ulinzi ujuzi na elimu kuhusu usalama wa taifa na uhusiano wa kimataifa.