Dar es Salaam, TANZANIA. Katika hafla iliyofanyika kwa njia ya mtandao kutokea Dar es Salaam hapo tarehe 30 April 2021, Balozi wa Marekani Dk. Donald J. Wright amekabidhi ruzuku kutoka katika Mfuko wa Balozi wa Marekani wa Kukabiliana na VVU/UKIMWI (AFHR) kwa asasi za kiraia na za kidini zipatazo 11 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania. Ruzuku hizi zitaelekezwa katika kutekeleza miradi ya ufuatiliaji inayolenga kuboresha huduma za kukabiliana na VVU nchini.
Fedha zinazotolewa kupitia ruzuku hizi hutolewa na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR), ambao ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya Serikali ya Marekani katika kukabiliana na janga la VVU/UKIMWI. Mpango huu ni mkubwa zaidi ya mpango wowote uliowahi kuendeshwa na nchi yoyote duniani katika kukabili ugonjwa wa aina moja. Toka kuanzishwa kwa PEPFAR hapo mwaka 2003, Serikali ya Marekani imechangia zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 5 katika kukabilianaa na VVU nchini Tanzania pekee.
Asasi zilizopatiwa ruzuku zilituma maombi, baada ya mfuko kukaribisha maombi ya maandiko miradi ya ufuatiliaji wa wanajamii wenyewe (Community-led monitoring – CLM) wa afua za kupambana na UKIMWI katika jamii zao. Miradi itakayotekelezwa italenga katika kuinua ubora wa huduma zinazohusu VVU kwa kukusanya data kuhusu matatizo, changamoto na vikwazo vinavyowakabili Watu wanaoishi na VVU, hususan, katika kuzifikia na kuzitumia huduma zitolewazo kwa watu wanaoishi na VVU. Aidha, miradi itafuatilia jinsi walengwa wanavyopokea na kuendelea (retention) na huduma katika vituo vya afya. Matokeo ya jitihada hizi za ufuatiliaji yatavisaidia sana vituo vya kutolea huduma na serikali za mitaa kufanya uboreshaji endelevu wa huduma zinazohusu VVU zitolewazo. Hii itaboresha viwango vya huduma na kufanya mchakato wake kuwa rahisi zaidi na ulio rafiki na unaowajali zaidi watu wanaoishi na VVU. Hatimaye, lengo kuu ni kuboresha maisha ya walengwa wa PEPFAR.
Mfuko wa Balozi wa kukabiliana na VVU/UKIMWI ulianzishwa mwaka 2009 na umeshatoa ruzuku kwa zaidi ya Asasi za kiraia 140, zisizojiendesha kibaishara nchini Tanzania. Serikali ya Marekani ina jivunia kuendeleza utamaduni wa kushirikiana na asasi hizi katika kufikia malengo ya Tanzania katika kudhibiti VVU/UKIMWI.
Wapokea Ruzuku kutoka katika Mfuko wa Balozi wa Kukabiliana na VVU/UKIMWI kwa mwaka 2021:
- Thubutu Africa Initiative (TAI), ambao wataondoa vikwazo vinavyowakabili watu wanaoishi na VVU katika kupata huduma za matunzo na matibabu katika Halmashauri ya Shinyanga, Mkoani Shinyanga.
- SIKIKA, ambao wataboresha upatikanaji na uwezo wa walengwa kuzifikia huduma bora za kinga na tiba kuhusu VVU katika wilaya ya Ukerewe, Mkoani Mwanza.
- Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS), kitashughulikia vikwazo vya utoaji huduma za afya katika Halmashauri ya Shinyanga, Mkoani Shinyanga.
- Integrated Rural Development Organisation (IRDO), itaimarisha utoaji huduma zinazohusu VVU katika Wilaya ya Nyasa, Mkoani Ruvuma.
- Women to Children Foundation (WOCHFO), itaboresha utoaji wa huduma za kinga na matibabu kuhusu VVU kwa kupitia ufuatiliaji unaofanywa na jamii katika Wilaya ya Ludewa, Mkoani Njombe.
- Kilimanjaro Women Information Exchange and Community Organisation (KWIECO), itaboresha upaatikanaji wa huduma za afya kwa watu wanaoishi na VVU katika wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro.
- Mtandao wa Wanawake Wanaoishi na VVU/UKIMWI (TNW+), utawatumia watu wanaoishi na VVU/UKIMWI ili kutoa elimu na kuboresha huduma za kukabiliana na VVU na Kifua Kikuu katika kata 25 za Wilaya ya Ukerewe, Mkoani Mwanza.
- STEPS Tanzania, itaboresha upatikanaji, utumiaji na ubora wa huduma za matunzo na matibabu miongoni mwa watu wanaoishi na VVU katika Wilaya ya Kisarawe, Mkoani Pwani.
- Education Outreach Tanzania (EDOTA) itaboresha utoaji wa huduma zinazohusu HIV katika vituo vya afya tisa katika Wilaya ya Mpanda, Mkoani Katavi.
- Agape AIDS Control Prograamme, itaaboresha mifumo ya kutoa mrejesho kwa watu wanaoishi na VVU na kuhimiza mabadiliko katika utoaji huduma za matunzo na matibabu katika vituo vya afya yatokanayo na datayofanyika kutokana na data katika wilaya ya Shinyanga, Mkoani Shinyanga.
- Community Development Trust Fund of Tanzania (CDTF), itajenga uwezo wa watoa huduma za Afya na zile zinazohusiana na VVU katika wilaya ya Kisarawe, Mkoani Pwani.
Kufahamu zaidi kuhusu Mfuko wa Balozi wa Kukabiliana na VVU/UKIMWI, wasiliana na Mratibu wa PEPFAR anayeshughulikia Asasi za Kiraia (Civil Society Outreach Coordinator) kwa barua pepe: PEPFARGrantsDar@state.gov