Jeshi la Marekani na Walinzi wa Mipaka watoa Mafunzo kwa Askari Wanyamapori wa Kitanzania 50

Major General Greg Lusk, Adjutant General for the North Carolina National Guard, speaking with U.S. Ambassador to Tanzania Mark Childress, Permanent Secretary of the Ministry of Natural Resources & Tourism Major General Gaudence Milanzi, and game scouts.
Jeshi la Marekani na Walinzi wa Mipaka watoa Mafunzo kwa Askari Wanyamapori wa Kitanzania 50
Jeshi la Marekani na Walinzi wa Mipaka watoa Mafunzo kwa Askari Wanyamapori wa Kitanzania 50

Hifadhi ya Wanyama ya Rungwa, TANZANIA.  Jumatano wiki hii, Balozi Mark Childress alishuhudia maonyesho ya mafunzo ya vitendo ya mbinu za medani yanayotolewa kwa askari wanyamapori wa Kitanzania ili kuinua uwezo wao wa kukabialiana na ujangili na usafirishaji haramu wa nyara za serikali katika Hifadhi ya Wanyama ya Rungwa.  Askari hawa wamekuwa wakishiriki katika mafunzo yanayotolewa na wataalamu wa kijeshi wa Kimarekani kutoka katika Kikosi Maalum cha Walinzi wa Mipaka kutoka North Carolina na Kikosi Maalumu cha Jeshi la Marekani Barani Afrika cha Pembe ya Afrika na kufadhiliwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Idara inayoshughulikia masuala ya Afrika.

Katika mafunzo yao ya wiki mbili yaliyoanza tarehe 25 Julai hadi tarehe 9 Septemba, askari wanyamapori wa Kitanzania wapatao 50 wanajifunza mbinu za upelelezi na doria, taratibu za  ukamataji na kuwashikilia watuhumiwa, utafutaji na ukamataji wa nyara, uchunguzi wa eneo lilipofanyika tukio la kihalifu, huduma ya kwanza, haki za binadamu na kanuni za medani.

Mnadhimu Mkuu wa Kikosi cha Walinzi wa Mipaka cha North Carolina Meja Jenerali Greg Lusk alisafiri kuja Tanzania kushuhudia mafunzo haya. Maonyesho ya Jumatano ya mafunzo ya mbinu za medani yalihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Jenerali Gaudence Milanzi; Mkurugenzi Mkuu wa Idara mpya ya Wanyamapori Tanzania, Martin Loibooki; Mkurugenzi wa Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa  Alex Songorwa; Meneja wa Mradi wa Hifadhi ya Rungwa Saidi Kabanda; na Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Kuhifadhi Wanyamapori  (Wildlife Conservation Society -WCS), Tim Davenport.

Mafunzo haya yalianzishwa mwaka 2015 baada ya Balozi Childress kutembelea Hifadhi ya Rungwa.  Baada ya kujionea mahitaji makubwa ya kujengea watendaji uwezo na kuboresha miundombinu ili kudhibiti ujangili ambao ulikuwa  umekithiri katika hifadhi hiyo, Balozi aliahidi kulishughulikia haraka suala hilo. Katika kipindi cha mwaka mmoja tu Balozi aliweza kuhamasisha wabia ambalimbali kuchangia katika kuwasaidia askari wanyamapori.  Alieleza kuwa michango ya wabia kama taasisi ya Wyss Foundation ambayo ilitoa vifaa na taa kwa askari wanyamapori katika mapori yaliyokuwa yamesheheni majangili, iliwezesha askari hao kufanya doria katika msimu wa masika kwa mara ya kwanza katika kipindi cha muongo mmoja. Katika tukio la Jumatano, Balozi Childress alisema, “Programu hii ni kielelezo cha ushirikiano imara uliopo kati ya Marekani na Tanzania na mfano wa kile tunachoweza kufanikisha tunapofanya kazi pamoja  yaani serikali, vyombo vya usalama, jumuiya ya kimataifa, asasi zisizo za Kiserikali, sekta binafsi na raia wa Tanzania nchini kote.”

Programu hii ni sehemu ya jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Marekani na wabia wake katika kulinda mapito ya tembo na wanyamapori wengine kati ya hifadhi za Rungwa na Katavi na hivyo kulinda mazingira ya eneo linalounganisha ikolojia ya Ruaha-Rungwa na ile ya Katavi.

Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo la Marekani (USAID) kwa kushirikiano na Taasisi ya Kuhifadhi Wanyamapori (WCS) linafadhili programu ya miaka mitano ya maeneo yaliyohifadhiwa katika nyanda za juu kusini na maeneo ya Ruaha-Katavi (SHARPP) itakayogharimu dola za Kimarekani milioni 8.5. Programu ya SHARPP italenga katika maeneo makuu manne ambayo ni kuimarisha maeneo ya jumuiya za hifadhi za wanyamapori (WMAs); kuimarisha hali ya maisha ya watu na vipato vyao katika maeneo yanayozunguka hifadhi; usimamizi bora wa maeneo wanapoishi wanyamapori (habitat management); na ufuatiliaji na ulinzi wa tembo. Mbali na mafunzo haya ya kuwajengea uwezo askari wanyamapori wa Rungwa, WCS kwa ufadhili wa USAID na wadau wengine kutoka sekta binafsi ilitoa mafunzo ya usimamizi wa eneo la tukio la kihalifu, Mfumo wa Ufuatiliaji na Utoaji Taarifa (the Spatial Monitoring and Reporting Tool – SMART) na mwitikio wa haraka katika kushughulikia tukio (rapid reaction).

Taarifa zaidi kuhusu ikolojia za Ruaha-Rungwa na Katavi zinapatikana katika tovuti zifuatazo:

http://www.tanzaniaparks.go.tz/

https://tanzania.wcs.org/Landscapes/Ruaha-Katavi.aspx

Kwa taarifa zaidi kuhusu tukio hili, tafadhali wasiliana kwa barua pepe na Japhet Sanga (SangaJJ@state.gov), Afisa Habari Mwandamizi wa Ubalozi wa Marekani, Dar es Salaam.