Dar es salaam- Leo wawakilishi kutoka Serikali ya Marekani na Serikali ya Tanzania walishiriki katika mkutano jumuishi katika viwanja vya Karimjee na wengine kupitia mtandao, ambapo wamesherehekea mafanikio na kujadili hatua itakayofuata katika kuhudumia watoto yatima na walio katika mazingira hatarishi na kuwawezesha vijana kupitia mradi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya kimataifa wa Kizazi Kipya. Dkt. Grace Maghembe Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI alihudhuria mkutano huu kama mgeni rasmi.
Makadirio ya watoto yatima nchini Tanzania ni milioni 3.2, na robo kati yao wenye miaka 5-14 wanafanya kazi, baadhi yao katika aina mbaya zaidi ya utumikishwaji wa watoto. Familia ni nguzo ya msingi katika kuwalinda watoto, lakini umaskini na magonjwa vinapunguza uwezo wa familia kuwahudumia watoto kikamilifu. Matokeo yake watoto wengi hususani walio chini ya miaka mitano wanakumbwa na magonjwa yanayoweza kuzuilika, udumavu na kuchelewa katika hatua za makuzi ya awali.
Mradi huu wa Kizazi Kipya kwa muda wa miaka mitano umetumia kiasi cha Dola za Marekani milioni 163.3 kuwawezesha watoto yatima na vijana wanaoishi na maambukizi pamoja na walezi wao kupata huduma stahiki zinazohusiana na UKIMWI kwa kuzingatia umri wao ili kuboresha hali zao za afya, lishe, elimu, ulinzi na usalama wa mtoto, ustawi wa maisha na ustawi wa kisaikolojia. Mradi uliamsha ari ya kutafuta huduma za UKIMWI, kupunguza vikwazo vya upatikanaji na utumiaji wa huduma za VVU na UKIMWI, na ufuatiliaji wa karibu kwa idadi ya watu waishio na virusi vya UKIMWI wanaositisha matumizi ya dawa. Kwa muda wa miaka mitano iliyopita Kizazi Kipya ilifanya kazi kwa ukaribu na Serikali ya Tanzania na Asasi zisizo za kiserikali kuwahudumia watoto yatima milioni 1.2 na takribani walezi 470,000 ili kuhakikisha kuwa vijana hawa wanapata huduma zinazohusiana na VVU na UKIMWI kulingana na umri wao na kupatiwa huduma ili kuboresha hali za maisha yao.
Kwa mfano, kupitia Kizazi Kipya zaidi ya vikundi vya kuweka na kukopa 12,200 vijulikanavyo kama WORTH Yetu viliundwa. Mpaka kufikia leo vikundi hivi vimeweza kukusanya jumla ya Shilingi za Kitanzania bilioni 26.6 sawa na dola za Kimarekani (milioni 11.6). Uwekaji wa akiba husaidia kupunguza vikwazo vya kiuchumi ambavyo mara nyingi huzuia watoto kupata huduma za msingi wanazozihitaji ili kuwa na afya bora na kuishi maisha bora.
Akizungumza katika hafla ya leo, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) V. Kate Somvongsiri alisema “watoto wanapokuwa na afya na ustawi bora, elimu na wakipata usaidizi kutoka kwa walezi na jamii zao, watakuwa na msingi na mbinu bora za kuwa vijana wazalishaji, na kuwa katika nafasi nzuri ya kufikia malengo yao. Hiki ndio kipaumbele kwa serikali zote mbili, serikali ya Tanzania na serikali ya Marekani.