Flag

An official website of the United States government

Marekani yatoa dozi nyingine milioni 1.6 za chanjo dhidi ya UVIKO-19 kwa Tanzania
3 MINUTE READ
Januari 19, 2022

Tanzania imepokea shehena nyingine ya zaidi ya dozi milioni 1.6 ya chanjo dhidi ya UVIKO-19 aina ya Pfizer BioNTech zilizotolewa na Serikali ya Marekani kupitia Mpango wa Kimataifa wa Usambazaji chanjo wa COVAX. Msaada huo ulipokelewa rasmi na Dk. Rashid Mfaume, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam aliyewakilisha Serikali ya Tanzania kutoka kwa Ananthy Thambinayagam, Mkurugenzi wa Ofisi ya Afya ya Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), katika hafla fupi iliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Kama sehemu ya jitihada zake za kulitokomeza janga hili duniani kote, hadi hivi sasa Serikali ya Marekani imeipatia Tanzania zaidi ya dozi milioni 4.5 za chanjo dhidi ya UVIKO 19.  Shehena ya kwanza kutoka Marekani iliyohusisha zaidi ya dozi milioni 1 za aina ya Johnson and Johnson ilipokelewa mwezi Julai 2021 na zaidi ya dozi milioni 3.5 za chanjo aina ya Pfizer BioNTech zilizoletwa kwa awamu tatu kati ya Novemba 2021 na Januari 2022. Misaada hii ni kielelezo cha ubia imara na dhamira ya dhati ya Serikali ya Marekani kwa watu wa Tanzania na malengo yetu ya pamoja ya kuushinda UVIKO-19 kwa pamoja.

Msaada wa Marekani katika jitihada za kimataifa za kukabiliana na UVIKO-19 unajumuisha:

  • Kuchangia dozi milioni 365 za chanjo kwa nchi nyingine.
  • Kununua dozi bilioni 1 za chanjo na kuzitoa kwa takriban nchi 100 zinazoendelea.
  • Kuchangia Dola za Kimarekani bilioni 4 kusaidia Mpango wa Kimataifa wa Usambazaji Chanjo COVAX, unaolenga kusambaza chanjo dhidi ya UVIKO-19 duniani kwa usawa na ufanisi.
  • Kusambaza dawa muhimu na vifaa tiba pamoja na kuzisaidia nchi kujenga upya uchumi wao, kukabiliana na upungufu wa chakula na kuimarisha usalama wa afya.

Rais wa Marekani Joe Biden ameahidi kuwa Marekani itakuwa ghala la dunia la chanjo dhidi ya UVIKO-19 katika mapambano ya pamoja dhidi ya janga hili. “Tutaendelea kufanya kila linalowezekana kuifanya dunia kuwa mahali salama zaidi dhidi ya kitisho cha magonjwa ya kuambukiza,” Alisema Rais Biden mwanzoni mwa mwaka huu.