Flag

An official website of the United States government

Ubalozi Wa Marekani Waendesha Mahafali Ya Programu Ya Mafunzo Ya Kiingereza Jijini Mwanza
4 MINUTE READ
Febuari 1, 2020

Ubalozi wa Marekani uliwatunukia vyeti wahitimu 25 wa programu maalumu ya mafunzo ya Kiingereza inayofadhiliwa na Ubalozi huo iitwayo English ‘Access’ Microscholarship Program iliyokuwa ikiendeshwa katika Chuo Kikuu cha Mt.Augustine (SAUT) jijini Mwanza.  Wanafunzi hao (wasichana 13 na wavulana 12) waliweza kuhitimu mafunzo ya miaka miwili ya Kiingereza ambapo walihudhuria madarasa ya lugha hiyo mara mbili kwa wiki baada ya muda wa kawaida wa masomo. Katika madarasa hayo, wanafunzi hao walijifunza pia maendeleo ya jamii na stadi za kuijumuisha jamii.  Ubalozi wa Marekani unafadhili madarasa haya katika maeneo mengine matano nchini Tanzania ambayo ni Mbeya, Lindi, Tanga, Unguja, na Pemba. Katika mwaka 2020, ubalozi utafungua madarasa zaidi katika miji ya Unguja, Tanga na kwa mara nyingine jijini Mwanza.

Akizungumza katika mahafali hayo, Afisa wa Ubalozi wa Marekani anayeshughulikia masuala ya umma, Brinille Ellis aliwapongeza wahitimu na wanafunzi wa Programu ya Access kwa kujitoa kwao kwa dhati na kujifunza kwa bidii. “Kupitia programu hii, sio tu mmeweza kupata umahiri wa lugha ya Kiingereza lakini pia mmekuwa viongozi na watu wa kupigiwa mfano katika jamii. Mmechukua mafunzo mliyoyapata darasani na kuyatekeleza katika miradi mbalimbali ya kujitolea ya maendeleo ya jamii na uhifadhi wa wanyama pori mliyoifanya.” Katika mahafali hayo, wanafunzi waliwasilisha kwa lugha ya Kiingereza kazi za kuhudumia jamii walizozifanya wakati wa mafunzo yao.

Programu ya Access hutoa mafunzo ya msingi ya lugha ya Kiingereza kwa watoto na vijana wenye vipaji wa kuanzia miaka 13 hadi 20 kutoka jamii zenye hali duni kiuchumi kupitia madarasa yanayoendeshwa baada ya muda wa shule na yanayotoa mafunzo ya kina. Programu ya Access huwapatia washiriki wake stadi za lugha ya Kiingereza jambo ambalo huwapa fursa zaidi za kielimu na ajira. Toka mwaka 2004, zaidi ya wanafunzi 350 kutoka Tanzania na 150,000 kutoka zaidi ya nchi 85 wameshiriki katika programu hii. Kwa maelezo zaidi, tembelea: https://americanenglish.state.gov/.