Flag

An official website of the United States government

Ubalozi wa Marekani watoa ruzuku ya Dola 52,540 kwa miradi ya kijamii
6 MINUTE READ
Novemba 2, 2021

Tarehe 2 Novemba, Naibu Balozi Robert Raines alisaini makubaliano ya kutoa ruzuku kwa miradi sita ya kijamii kupitia mfuko wake wa kusaidia miradi ya maendeleo inayoendeshwa na wanajamii wenyewe (Special Self-Help Program).

Mfuko Maalum wa Balozi wa kusaidia miradi ya maendeleo inayoendeshwa na wanajamii wenyewe umekuwa ukiwasaida Watanzania kuendeleza jamii zao toka mwaka 1965.  Mfuko huu husaidia miradi midogo midogo ya maendeleo ya jamii inayoendeshwa na jamii zenyewe nchini kote Tanzania.

Kwa mujibu wa Naibu Balozi Raines, Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Miradi ya Kijamii, ni programu muhimu inayoiwezesha Marekani kushirikiana moja kwa moja na vikundi vya kijamii vinavyofanya kazi kwa bidii kuleta maendeleo na mabadiliko chanya katika jamii zao.

“Ninaamini mabadiliko ya kweli na ya kudumu hutokea pale ambapo watu katika ngazi ya chini kabisa wanaposhirikiana kuleta mabadiliko chanya katika jamii zao,” alisema Naibu Balozi Raines.

Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Miradi ya Kijamii ulianzishwa ili kuvisaidia vikundi ambavyo vimeonyesha dhamira ya dhati ya kujiletea maendeleo. Kwa zaidi ya miaka 50 mfuko huu umesaidia miradi midogo midogo ya maendeleo ya jamii katika kila mkoa wa Tanzania.

Orodha ya taasisi/vikundi vilivyopata ruzuku mwaka huu:

Ruzuku Kutoka Mfuko wa Balozi wa Miradi ya Kijamii

Asasi:  Agro-Livestock and Welfare Advancement Rural Environment (AWARE)
$9,692
Mradi huu unalenga kujenga mfumo wa kuvuna maji ya mvua katika zahanati 4 katika wilaya ya Kalambo, Mkoani Rukwa. Mradi huu utatatua tatizo la upatikanaji maji kwa jamii, hususan kwa vijana, wanawake, watu wenye ulemavu na watu wanaoishi na VVU. Kupitia mradi huu, matanki manne ya kuvuna maji ya mvua yatajengwa katika zahanati za Msanzi, Mkali, Katazi na Kasanga, kila tanki likiwa na uwezo wa kuchukua maji lita 20,000 yatakayokuwa yakikusanywa kutoka katika mapaa ya zahanati hizo.

Asasi: Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania – Mradi wa Bega kwa Bega
$10,634.27
Mradi wa Bega kwa Bega wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania unashirikiana na Asasi ya Kimarekani iitwayo Saint Paul Partners,ambayo ina uzoefu wa zaidi ya miaka 19 katika utekelezaji wa miradi ya maji mkoani Iringa.  Lengo la mradi huu ni kukipatia Kijiji cha Magome, Mkoani Iringa, maji safi na salama. Mradi huu unalenga kupeleka maji katika maeneo matatu yaliyoainishwa na wanakijiji wenyewe: shule ya msingi, zahanati na eneo la soko na kanisa la Kilutheri kupitia mfumo wa usambazaji maji wa mteremko (gravity-fed system).

Naibu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Robert Raines akimkabidhi mwakilishi wa Asasi ya Disability Relief Services – Tanzania kutoka mkoani Kigoma, Jeremiah Mutagoma hati ya makubaliano ya ruzuku.
Naibu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Robert Raines akimkabidhi mwakilishi wa Asasi ya Disability Relief Services – Tanzania kutoka mkoani Kigoma, Jeremiah Mutagoma hati ya makubaliano ya ruzuku.

Asasi: Disability Relief Services – Tanzania (DRS-Tanzania)
$9,781
Lengo la mradi huu ni kuona watu wenye ulemavu, hususan vijana na wanawake katika mkoa wa Kigoma wanashiriki katika ukulima wa kisasa kwa kufuga mbuzi wa kisasa na kuzalisha mazao ili kupata chakula chao na malisho ya mifugo yao hivyo kuboresha lishe, kuinua usalama wa chakula na kujiongezea kipato kupitia kilimo.

Asasi: Prophina Day Care Centre
$9,994.65
Mradi huu unalenga kuinua elimu na kukabiliana na kutokujua kusoma na kuandika kwa kujenga madarasa mawili ya ziada yatakayowawezesha watoto wengi zaidi walio chini ya umri wa kwenda shule, kupata mazingira ya kujifunzia na hivyo kuwapa wazazi wao nafasi ya kwenda kufanya shughuli nyingine nje ya nyumbani. Kituo hiki kina lengo la muda mrefu la kuwa Shule ya Msingi ifikapo mwaka 2024.

Asasi: Olive Branch for Children
$2,703.03
Lengo la mradi huu ni kuelimisha jamii ya Usangu kuhusu utunzaji endelevu wa mazingira kwa kupanda miti na kutayarisha vitini vya kutolea elimu.

Asasi:  Jumuiya ya Maendeleo Unguja Ukuu (Unguja Ukuu Development Organisation – JUMAU)
$9,735.05
Kukuza elimu kwa kujenga jengo la madarasa katika Shule ya Msingi Ukuu. Jengo hii litaongeza madara matatu katika shule hii hivyo kuwawezesha wanafunzi wengi zaidi kuhudhuria shuleni katika wakati mmoja.