DAR ES SALAAM, TANZANIA, 18 Novemba, 2020 – Leo hii, Balozi Donald Wright alisaini makubaliano ya kutoa ruzuku kwa miradi sita ya kijamii kupitia mfuko wake wa kusaidia miradi ya maendeleo inayoendeshwa na wanajamii wenyewe (Self-Help Program) pamoja na miradi inayopata ruzuku kutoka mifuko mbalimbali ikiwemo Mfuko wa Demokrasi Afrika (the Africa Regional Democracy Fund), Mfuko wa Taasisi ya Julia Taft na Mfuko wa Ubunifu katika Kuhakikisha Uwazi katika masuala ya fedha za umma (Fiscal Transparency Innovation Fund).
Mfuko Maalum wa Balozi wa kusaidia miradi ya maendeleo inayoendeshwa na wanajamii wenyewe umekuwa ukiwasaida Watanzania kuendeleza jamii zao toka mwaka 1965. Mfuko huu hutoa ruzuku ndogo ndogo hutolewa kusaidia miradi inayoendeshwa na vikundi na taasisi za kijamii kuendesha miradi ya kujiongezea kipato Pamoja na miradi ya maendeleo endelevu katika kila mkoa nchini Tanzania.
“Ninaamini mabadiliko ya kweli nay a kudumu hutokea pale ambapo wananchi katika ngazi ya chini kabisa hujiunga Pamoja na kuleta mabadiliko chanya katika jamii zao,” alisema Balozi Wright katika hafla fupi ya kukabidhi ruzuku iliyofanyika nyumbani kwake jijini Dar es Salaam.
Mbali na miradi hiyo sita iliyopata ruzuku kutoka katika mfuko wa Balozi, Balozi Wright alikabidhi pia ruzuku kwa taasisi nyingine tatu zinazoendesha miradi inayolenga kuongeza uwazi, utawala bora, ushiriki wa vijana katika kuisimamia serikali, kusaidia uwezeshaji wa wanawake na wasichana katika jamii za wakimbizi na kuboresha uwezo wa wanasheria kutoa huduma kwa maslahi ya jamii.
Orodha ya Vikundi/Taasisi/Asasi zilizopatiwa Ruzuku
Ruzuku kutoka Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Miradi ya Kijamii
Taasisi: Agricultural and Livestock Production Development Association (ALPDA)
Kiasi cha Ruzuku: Dola za Kimarekani 8,794.94
Mahali: Dodoma
Mradi huu unalenga kuboresha uwezo wa wanawake na vijana kujiongezea kipato, ukiwalenga hususan vijana walio nje ya mashule na wanawake wanaojihusisha na ukulima mdogo mdogo wa karanga katika vijiji vya Veyula, Miyuji na Makutupora kwa kununua mashine tatu za kutengenezea siagi ya karanga na kutoa mafunzo ya kuzitumia mashine hizo kwa wanawake na wasichana 40 kutoka kila kijiji.
Taasisi: Thubutu Africa Initiatives (TAI)
Kiasi cha Ruzuku: Dola za Kimarekani 7,395.13
Mahali: Shinyanga
Mradi huu unalenga kuelimisha kuhusu tabia zitakazowawezesha vijana kulinda na kuboresha afya zao na kuinua mahudhurio ya wasichana shuleni kwa kujenga vyoo nane, ikiwemo vyoo Rafiki kwa wanafunzi wenye ulemavu na kujenga vituo vya kunawia mikono kwa wasichana na wavulana.
Taasisi: Kayaga for Social Economic Group (KASEG)
Kiasi cha Ruzuku: Dola za Kimarekani $6,500
Mahali: Mwanza
Mradi huu unalenga kuinua kipato cha wachuuzi wadogo wadogo wa dagaa wapatao 105 kwa kununua mashine ya kisasa ya kukaushia samaki na vifungashio vya kisasa ili kuwawezesha kukausha, kufungasha na kuweka lebo bidhaa zao kwa usafi, unadhifu na kwa haraka hata wakati wa msimu wa mvua.
Taasisi: PVL (Plantation, Vendors and Livestock) Group
Kiasi cha Ruzuku: Dola za Kimarekani $9,864
Mahali: Njombe
Mradi huu unalenga kutoa elimu na kutanzua changamoto ya kutokujua kusoma na kuandika kwa kujenga kituo cha elimu na kuendesha madarasa kutoka kijiji hadi kijiji wakihamasisha wazazi, vijana na wazee kujiendeleza kielimu, Pamoja na kuchukua data kuhusu mahitaji ya watu.
Taasisi: Shirika La Maendeleo Ya Kilimo Na Ufugaji Musoma
Kiasi cha Ruzuku: Dola za Kimarekani 9,955.42
Mahali: Mara
Mradi huu unalenga kuinua kipato cha wakulima wadogo wa alizeti wilayani Musoma kwa kuimarisha uzalishaji wa zao hilo, kukamua mafuta na kuyachakata (processing) kwa kununua mashine ya kukamua, kusafisha na kuchuja mafuta ya alizeti. Aidha, mradi utanunua vifungashio vya bidhaa zao pamoja na kutoa mafunzo kwa wakulima ya namna ya kutumia mashine hizo.
Taasisi: Maji Safi kwa Afya Bora Ifakara (MSABI)
Kiasi cha Ruzuku: Dola za Kimarekani: 5,022.75
Mahali: Morogoro
Kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa kuboresha mifumo ya usimamizi wa fedha na uendelevu wa vituo cha kuchotea maji kwa kutumia mfumo uuitwao “Pump for Life maintenance system”, unaofanya matengenezo ya vifaa kila mara kwa ada ya kila mwezi.
Ruzuku kutoka Mfuko wa Kuongeza Uwazi katika Usimamizi wa Fedha (Fiscal Transparency Innovation Fund)
Taasisi: WAJiBU Institute of Public Accountability
Kiasi cha Ruzuku: Dola za Kimarekani
125,000
Mradi huu unalenga kuinua uwazi na uwajibikaji nchini Tanzania kwa kuongeza ushiriki/ ushirikishwaji wa vijana katika mchakato wa kutayarisha bajeti. Malengo ya mradi ni Pamoja na kuongeza uweza wa vijana kupata taarifa kuhusu uwajibikaji kwa umma kwa kutoa machapisho yaliyo Rafiki kwa vijana ili kuinua uelewa wao kuhusu namna serika inavyotumia rasilimali pamoja na kuangazia mapendekeo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).
Ruzuku kutoka Mfuko wa Demokrasia Afrika (Africa Regional Democracy Fund – ARDF)
Taasisi: Centre for Strategic Litigation
Kiasi cha Ruzuku: Dola za Kimarekani 136,000
Programu hii inalenga kuinua uwezo wa wanasheria vijana kutoka Tanzania, Kenya na Uganda kusimamia mashauri yenye maslahi ya umma ili kutetea demokrasia na haki za binadamu kwa kutoa mafunzo ya ziada ya namna ya kusimamia na kutoa utetezi katika kesi au mashauri yanayohusu uhuru wa msingi wa watu.
Mfuko wa Taasisi Julia Taft
Taasisi: Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake (Women’s Legal Aid Centre)
Kiasi cha Ruzuku: Dola za Kimarekani 25,000.00
Mradi huu unalenga kutoa elimu kuhusu usafirishaji haramu wa binadamu, sheria zinazohusiana na tatizo hili na haki za waathiriwa wa usafirishaji haramu wa binadamu. Mradi huu utahusisha kuwajengea uwezo wasimamizi wa sheria katika ngazi ya makambi ya wakimbizi Pamoja na jamii za wakimbizi ili kuinua uelewa wao kuhusu vyanzo vya tatizo hili pamoja na kutambua njia mbalimbali za ufumbuzi wake.