Tamko la Ubalozi wa Marekani kuhusu uchaguzi Zanzibar

Serikali ya Marekani imestushwa sana na tamko la hivi karibuni la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ambapo ametamka kusudio lake la kufuta matokeo ya uchaguzi wa urais wa Zanzibar. Hatua hii inasitisha mchakato wa uchaguzi uliofanyika vizuri na kwa amani, kama ilivyo elezwa na waangalizi wa uchaguzi kutoka Ubalozi wa Marekani, Jumuiya ya Ulaya, Jumuiya ya Madola na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika pamoja na kusitisha zoezi la majumuisho ya kura lililokuwa linakaribia kukamilika. Tunatoa wito wa kuondolewa kwa tamko hilo  na kuzisihi pande zote kudhamira kwa dhati kuukamilisha mchakato huu wa kidemokrasia kwa uwazi na kwa Amani. Watu wa Zanzibar wanastahili jambo hilo.