Flag

An official website of the United States government

Ubalozi wa Marekani wasaidia Wajasiriamali Wanawake Zanzibar
4 MINUTE READ
Juni 28, 2021

Zanzibar – Wajasiriamali wanawake 17 kutoka Zanzibar, leo wanahitimu mafunzo maalumu ya wiki 13 katika biashara na ujasiriamali yaliyofadhiliwa na serikali ya Marekani kupitia programu yake ya kuwajengea uwezo wajasiriamali wanawake (Academy of Women Entrepreneurs – AWE). Katika mahafali yao yaliyohudhuriwa na Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mama Zuhura Kassim, wanawake hawa wajasiriamali walipongezwa na kuhimizwa kuendelea na kuboresha shughuli zao za uzalishaji mali na kujiongezea kipato. Ubalozi wa Marekani uliwakilishwa na Balozi Mdogo Bi. Amy Hart Vrampas.

AWE ni mpango wa Kimataifa wa Serikali ya Marekani wa kuwawezesha wanawake kiuchumi unaokusudia kuwajengea uwezo wanawake milioni 50 duniani kote kufikia upeo wa uwezo wao kiuchumi. AWE ina dhamira ya dhati ya kuwapa wanawake elimu na ujuzi, kuwajengea mitandao na kufungua fursa wanazohitaji ili kuyabadilisha mawazo yao kuwa miradi halisi ya kujiletea kipato.

Akizungumza na wahitimu katika mahafali hayo, Bi. Vrampas alielezea matokeo ya mafunzo yanayotolewa na AWE. “Mafunzo ya wiki 13 mliyoyapata mkiwa sehemu ya programu hii yamewapa ujuzi kwa vitendo utakaowawezesha kuanzisha biashara endelevu pamoja na kuwaunganisha na wakufunzi (mentors) na wajasiriamali kama ninyi wa nchini Marekani,” alisema.

Aliendelea kusema kuwa kuwajengea wanawake uwezo wa kiuchumi ndio njia ya haraka zaidi ya kuibadilisha jamii. “Jitihada za wanawake huwa na matokeo makubwa zaidi kwa jamii nzima kwa sababu wanawake wanapofanikiwa mara nyingi watawekeza mapato yao katika familia na jamii zao, wakigharamia mahitaji kama vile ada kwa watoto wao na huduma za afya.  Manufaa ya kiuchumi ya mafanikio yenu yanasaidia vizazi vijavyo. Tayari ubunifu wenu unaleta matokeo chanya katika jamii na uchumi wa Tanzania,” alisema.

Kundi la wahitimu wa Zanzibar ni kundi la tatu la washiriki wa programu ya AWE.  Kundi la kwanza la wanawake 20 lilihitimu tarehe 9 Septemba, 2019 jijini Dar es Salaam. Kundi la pili lililokuwa na wanawake wajasiriamali 25 kutoka Iringa lilihitimu tarehe 16 Desemba 2020.  Awamu ya nne ya mafunzo ya AWE nchini Tanzania yatafanyika Mwanza, kuanzia Julai 2021.

Kupitia Taasisi ya Marekani ya Maendeleo ya Afrika (U.S. African Development Foundation -USADF), wajasiriamali wanaoshiriki programu ya AWE wanaweza kupatiwa na USADF fedha za mtaji wa hadi Dola za Kimarekani 25,000 ili kupanua biashara zao.

Ubalozi wa Marekani unashirikiana na Selfina kutekeleza programu ya AWE nchini Tanzania. Ikiwa imeanzishwa mwaka 2002 na Dk. Victoria Kisyombe, Selfina ni taasisi ya Kitanzania ya utoaji mikopo midogo midogo iliwalenga zaidi akina mama wajane na wasichana. Katika miaka 19 iliyopita, Selfina imewawezesha kiuchumi zaidi ya wanawake 31,000 kupitia mikopo inayozunguka. Maisha ya zaidi ya watu 300,000 yamegushwa kutokana na faida zilizopatikana kutokana na mikopo hiyo. Wanawake sasa ni wamiliki wa biashara zao wenyewe na zaidi ya nafasi za ajira 150,000 zimetengenezwa.