Serikali Ya Marekani Yatangaza Mpango Mpya Wa Kusaidia Elimu Kwa Watoto Wa Kike Nchini Tanzania

Serikali Ya Marekani Yatangaza Mpango Mpya Wa Kusaidia Elimu Kwa Watoto Wa Kike Nchini Tanzania
Serikali Ya Marekani Yatangaza Mpango Mpya Wa Kusaidia Elimu Kwa Watoto Wa Kike Nchini Tanzania
Serikali Ya Marekani Yatangaza Mpango Mpya Wa Kusaidia Elimu Kwa Watoto Wa Kike Nchini Tanzania

Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) limetangaza hivi leo programu mpya nchini Tanzania inayolenga kuongeza fursa na ubora wa elimu kwa watoto wa kike. Tangazo hili linafuatia tukio la maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike lililofanyika tarehe 11 Oktoba katika Ubalozi wa Marekani ambapo wasichana 50 wa Kitanzania waliungana na Mke wa Rais wa Marekani Michelle Obama katika majadiliano kwa njia ya mtandao kuhusu elimu kwa wasichana.  Programu hii mpya nchini Tanzania ni sehemu ya mpango uitwao “Let Girls Learn uliozinduliwa na Rais Barack Obama na Mama Michelle Obama hapo mwaka 2015 kwa lengo la kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakwamisha wasichana kupata elimu bora itakayowawezesha kufikia upeo wa uwezo wao.

Sambamba ya tangazo hili, USAID nchini Tanzania ilitangaza kuwa itasaini makubaliano ya ushirikiano na Shirika la Global Affairs Canada (GAC) katika kuutekeleza mpango huo. Makubaliano haya yanajengwa katika ushirikiano ambao umekuwepo kati ya USAID na GAC kupitia Kundi la Wabia wa Maendeleo ya Elimu linaloshirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya Tanzania katika kuandaa Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu na sera za elimu. Katika makubaliano haya, taasisi hizi zimeazimia kushirikiana katika kuainisha maeneo yakayowezesha upatikanaji wa elimu bora, uboreshaji wa mazingira wezeshi kwa wasichana kupata elimu bora na kuwawezesha wasichana kuwa mawakala wa mabadiliko.

Toka kuanzishwa kwa mpango wa Let Girls Learn, USAID imewekeza zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 600 katika programu mbalimbali zinazoendeshwa chini ya mpango huu katika nchi 13 barani Afrika, Mashariki ya Kati, Asia na Amerika ya Kusini. Katika nchi za Tanzania na Malawi ambazo ni nchi za kipaumbele katika mpango huu, Serikali ya Marekani itawekeza hadi Dola za Kimarekani milioni 25 ikifanya kazi na wabia mbalimbali kupata mbinu bora na za kibunifu za kuboresha elimu kwa wasichana.

Hapa Tanzania,  Shirika liitwalo World Education ndilo litakaloendesha mpango huu, utakaojulikana kwa Kiswahili kama “Waache Wasome,” ambao msingi wake utajengwa katika jitihada za muda mrefu za USAID za kuwajengea uwezo wanawake vijana. Kwa kushirikiana na asasi mbalimbali zikiwemo Restless Development, WGBH Educational Foundation na Campaign for Female Education (Kampeni kwa ajili ya elimu ya mwanamke), mpango wa Waache Wasome utaongeza kiwango cha kuandikishwa shuleni na kuendelea kubaki shuleni kwa wasichana wenye umri wa kati ya miaka 13 – 19 na kubadilisha mitazamo ya jamii kuhusu thamani ya kuwaelimisha wasichana katika wilaya zilizochaguliwa katika mikoa ya Arusha na Mara. Mradi huu ulitokana na warsha ya USAID iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Mei, ambapo kwa pamoja wataalamu wa maendeleo, wafadhili na maafisa wa serikali za Tanzania na Malawi waliandaa mbinu bunifu za kuwasaidia watoto wa kike kupata elimu bora.

“USAID nchini Tanzania inafahari kubwa kuwa sehemu ya mpango wa Let Girls Learn, ambao unaimarisha mkakati wetu wa kusaidia kuinua hali ya kijamii na kiuchumi ya Tanzania hususan kwa kuwajengea uwezo wanawake na vijana,” alisema Mkurugenzi wa USAID nchini Sharon Cromer. “Tumedhamiria kwa dhati kuboresha stadi za kujifunza katika kipindi chote cha maisha miongoni mwa Watanzania, hasa wale walio katika makundi yanayowekwa pembezoni na kukosa haki nyingi za kimsingi kama wasichana ambao wanakabiliwa na vikwazo vingi vinavyowakwamisha wasipate elimu.”

Wakati ambapo viwango vya uandikishaji shuleni watoto vya kike na wa kiume nchini Tanzania havitofautiani, bado vikwazo kama ndoa za utotoni huwakwamisha wasichana wengi kupata fursa ya elimu. Pungufu ya asilimia 20 ya wanawake wenye umri wa kati ya miaka 20-24 ndio wamemaliza shule za sekondari na asilimia 20 hawakupata elimu kabisa. Mpango mpya wa Waache Wasome  utamchukulia na kumhudumia msichana kwa ukamilifu wake (whole-of-girl approach) kwa kupunguza vikwazo vinavyomkabili vinavyomfanya asiweze kuandikishwa shuleni au kuendelea na masomo yake shuleni huku ukishughulikia pia vikwazo vinavyomkabili akiwa nyumbani na katika jamii. Aidha, mpango utaongeza ushirikiano kati ya sekta za elimu, afya na ustawi wa jamii katika kumhudumia mlengwa. Kwa kuzishirikisha kikamilifu jamii, ikiwa ni pamoja na wazazi, wanaume, walimu na wavulana, mpango huu unalenga kubadilisha mitazamo ya kijinsia na kuongeza kiwango cha jamii na familia cha kuthamini elimu kwa wasichana.  Hali kadhalika, mpango wa “Waache Wasome” unalenga kuwajengea uwezo wasichana na kupunguza ndoa na mimba za utotoni.

Makubaliano mapya ya ushirikiano kati ya Marekani na Kanada katika kutekeleza shughuli za mpango huu yanalenga kuongeza matokeo na manufaa ya jitihada na misaada ya nchi hizi mbili katika kusaidia elimu. Makubaliano haya ni kielelezo cha dhamira yetu ya dhati ya kupanua fursa za elimu kwa kuzingatia vipaumbele vya serikali ya Tanzania katika sekta ya elimu.

“Kanada inafurahi kufanya kazi na USAID nchini Tanzania katika kuboresha na kupanua fursa za elimu kwa wasichana  kwa kutanzua vikwanzo vinavyowakwanisha wasipate elimu bora na kuwajengea uwezo wa kuwa viongozi,” alisema  Balozi wa Kanada nchini Ian Myles. “Hivi sasa msaada wa Kanada umeelekezwa zaidi katika kuinua ubora wa elimu katika shule za msingi na sekondari kwa kuinua ubora wa elimu kwa walimu. Kanada itafanyakazi na Serikali ya Marekani katika kuhakikisha kuwa masuala yanayowaathiri wasichana yanaibuliwa na kujadiliwa katika majadiliano ya kisera na Serikali ya Tanzania.”

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Afisa Habari Msaidizi, Jacqueline Mosha (MoshaJP@state.gov)