Flag

An official website of the United States government

Serikali ya Marekani yatangaza kuanza kwa Programu ya Diversity Visa
4 MINUTE READ
Oktoba 6, 2021

Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam unatangaza kuanza kwa programu ya Diversity Visa kwa mwaka 2023 (DV-2023) hapo tarehe 6 Oktoba 2021.  Kila mwaka, kupitia programu hii, Marekani hutoa viza za ukaazi wa kudumu (immigrant visas) zipatazo 55,000 kwa raia wa nchi ambazo kihistoria zina idadi ndogo ya watu wanaohamia Marekani. Mwaliko unatolewa kwa Watanzania wenye sifa kutuma maombi yao katika programu hii ya uhamiaji kabla ya tarehe 9 Novemba 2021.

Tafadhali soma kwa makini na kwa ukamilifu maelekezo ya namna ya kutuma maombi yako kupitia tovuti maalumu; https://travel.state.gov/content/travel/en/us-visas/immigrate/diversity-visa-program-entry/diversity-visa-instructions.html. Maombi ya kupata viza hiyo katika kipindi cha mwaka 2023 (DV-2023) yatapokelewa kuanzia tarehe 6 Oktoba, saa 6 mchana kwa saa za Marekani Mashariki (EST) hadi tarehe 9 Novemba 2021 saa 6 mchana kwa saa za Marekani Mashariki (EDT). Tuma maombi yako kwa kujaza fomu maalumu ya kielektroniki ya kuomba kushiriki katika programu ya Diversity Visa (E-DV Entry Form au DS-5501) inayopatikana kupitia dvprogram.state.gov. Unaweza kutuma ombi lako mara moja tu, katika kipindi kilichotajwa na kwa njia ya mtandao pekee.  Maombi yaliyochelewa au yatakayoletwa kwa njia ya barua/karatasi hayatapokelewa.

Tafadhali zingatia taarifa muhimu zifuatazo:

  • Hakuna ada yoyote inayotozwa kwa kutuma maombi yako kupitia mtandao. Tafadhali usitume, usilipe wala kuhamishia fedha kwa taasisi au mtu yeyote anayedai anaweza kukusaidia kupata viza hii.
  • Ni lazima uingie katika mtandao wa Internet ili uweze kujua kama utakuwa umechaguliwa kuendelea na mchakato wa visa hii. Mfumo wa kueleza matokeo ya Diversity Visa utapatikana katika tovuti ya dvprogram.state.gov kuanzia tarehe 8 Mei 2022, hadi angalau tarehe 30 Septemba 2023
  • Iwapo utakuwa umepata Diversity Visa, utatakiwa tu kulipia ada ya maombi ya viza katika Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam wakati utakapoitwa kwa ajili ya usaili wa viza. Iwapo kuna mtu yeyote atakayekudai fedha kwa ajili ya kukusaidia kuingia katika Programu hii, tafadhali wasiliana na Ubalozi wa Marekani.
  • Kuchaguliwa kwa maombi yako ya Diversity Visa, hii haikuhakikishii moja kwa moja kupata viza. Endapo maombi yako ya Diversity Visa yatachaguliwa, bado utahitajika kusailiwa ili kuona kama unakidhi vigezo vya sheria ya Uhamiaji wa Marekani.
  • Unaweza kuwajumuisha watu wa familia yako (mke/mume na watoto wako wa kuwazaa ambao bado hawajaoa au kuolewa walio chini ya miaka 21) katika maombi yako ya Viza hii.  Iwapo utaongeza watu wengine (mbali na hao waliotajwa) maombi yako ya Viza yatakataliwa.  Iwapo mtu yeyote atakuomba ujumuishe watu wengine katika maombi yako ya visa, tafadhali wasiliana na Ubalozi wa Marekani – si lazima utaje jina lako utakapotupatia taarifa hiyo.
  • Orodhesha watu wote wa familia yako (immediate family) katika maombi yako hata kama watu hao wasingependa kuhamia Marekani pamoja nawe. Kushindwa kufanya hivyo kutasababisha wewe kukosa sifa na maombi yako kukataliwa wakati wa usaili wa viza.

Iwapo utakuwa na maswali zaidi, tafadhali yatume kwa barua pepe: drsiv@state.gov