Serikali Ya Marekani Yatoa Wito Kwa Serikali Ya Tanzania Kupanua Uwekezaji Katika Upatikanaji Wa Madawa Na Vifaa Tiba

A health care worker conducts physical inventory in a health facility in Kinondoni District.
Serikali Ya Marekani Yatoa Wito Kwa Serikali Ya Tanzania Kupanua Uwekezaji Katika Upatikanaji Wa Madawa Na Vifaa Tiba
Serikali Ya Marekani Yatoa Wito Kwa Serikali Ya Tanzania Kupanua Uwekezaji Katika Upatikanaji Wa Madawa Na Vifaa Tiba

1 Juni, 2016 – Akizungumza jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuhitimishwa kwa mradi wa usimamizi bora wa manunuzi na ugavi wa madawa na vifaa tiba (Supply Chain Management System – SCMS) na mradi wa USAID/DELIVER, Mkurugenzi wa Ofisi ya Afya wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Janean Davis alisisitiza umuhimu wa Serikali ya Tanzania kuweka kipaumbele katika upatikanaji wa madawa na vifaa tiba na katika mfumo wa kitaifa wa upatikanaji na ugavi wa madawa na vifaa tiba (national public health supply chain). Hafla hii ilitumika pia kuadhimisha miaka 10 ya jitihada za kuimarisha mfumo wa ugavi wa madawa na vifaa tiba nchini Tanzania na kuonyesha mafanikio makubwa ambayo miradi hii imeyafikia ambayo yatatoa msukumo mkubwa katika usimamizi wa ugavi madawa na vifaa tiba.

“Kwa niaba ya USAID, nafurahishwa kwamba Serikali ya Tanzania imetenga fedha kwa ajili ya madawa na vifaa tiba. Aidha, ninatoa wito kwa wizara mbalimbali zilizowakilishwa hapa hivi leo kuhakikisha kuwa fedha zilizotengwa katika bajeti zenu kwa ajili ya masuala ya afya zinatolewa na kuelekezwa kule zilikokusudiwa,” alisema Davis. “Mtandao wa uhakika na wenye uwazi wa usambazaji na ugavi wa madawa na vifaa tiba ni mojawapo ya mambo muhimu sana katika kuwawezesha Watanzania kuwa na afya bora na hivyo kujenga Tanzania yenye ustawi katika siku zijazo.”

Kwa kipindi cha muongo mmoja uliopita, Miradi ya SCMS na USAID | DELIVER kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Wizara ya Afya ya Zanzibar pamoja na wadau wengine, imekuwa ikinunua  madawa na vifaa tiba na kutoa msaada wa kitaalamu katika kuufanya mfumo wa manunuzi na ugavi wa madawa na vifaa tiba wa Tanzania kuwa wenye tija na ufanisi zaidi.

Msaada huu wa kitaalamu uliwezeshwa na USAID chini ya ufadhili wa Mpango wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) na Mpango wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Malaria. Hadi ilipofika mwezi Machi 2016, miradi hii kwa pamoja, ilikuwa tayari imewekeza zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 466 katika kuimarisha mfumo wa ugavi wa madawa na vifaa tiba nchini Tanzania  ikiwa ni pamoja na manunuzi ya madawa na vifaa tiba vya kukabiliana na VVU/UKIMWI, malaria na maradhi mengine ya zaidi ya Dola za Kimarekani milioni $375. Kiasi hiki kinajumuisha pia Dola milioni 67 zilizotumika katika madawa na vifaa tiba kwa ajili ya afya ya uzazi.

Miradi hii imekuwa na matokeo yanayojionyesha wazi katika ngazi zote kuanzia usimamizi wake katika ngazi ya kitaifa hadi kwa watumiaji wa huduma zake katika takriban vituo 5,000 vya utoaji huduma nchini kote Tanzania. Miongoni mwa matokeo hayo ni kuimarika kwa matumizi ya takwimu katika kufanya maamuzi; kuhakikisha ubora wa dawa kwa kuboresha uhifadhi wake na mifumo ya upatikanaji na usambazwaji wake (commodity management practices); na kuboreshwa kwa uwezo wa kitaasisi (organizational capacity) wa kuusimamia kwa ufanisi mfumo wenyewe.

Katika mjadala uliofanyika wakati wa hafla hii, mada kuu mbili zilijitokeza, nazo ni uimarishwaji wa mifumo katika ngazi ya serikali za mitaa na umiliki wa nchi (country ownership) wa mifumo hii. Wadau mbalimbali waliwasilisha mafunzo waliyoyapata kuhusu yale yanayoweza kufanyika ili kuimarisha mifumo ya utoaji huduma za afya hususan katika kuhakikisha kuwa kuna mfumo wa ugavi wa madawa na vifaa tiba wenye ufanisi na wenye uwajibikaji. Aidha, maonyesho yaliyofanyika kabla ya hafla yenyewe yaliwapa fursa washiriki kujadili njia bora zaidi ya kujenga uwezo wa kuisimamia na kuiendeleza mifumo hii.

“Miradi hii imefanya kazi bega kwa bega na Wizara katika kuimarisha mfumo wa utoaji huduma za afya wa Tanzania kwa kutoa ufumbuzi wa kibunifu na endelevu katika ugavi wa madawa na vifaa tiba,” alisema Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Mpoki Ulisubisya. “Leo tunaungana pamoja katika kutafakari ubia wetu wa muongo mmoja uliowezesha kuimarisha mifumo ya ugavi wa madawa hivyo kuokoa maisha ya watu Tanzania bara na Zanzibar.”

Kwa taarifa zaidi kuhusu hafla hii, tafadhali wasiliana kwa barua pepe na Japhet Sanga (SangaJJ@state.gov), Afisa Habari Mwandamizi wa Ubalozi wa Marekani, Dar es Salaam.