Dodoma:
Januari 23, 2020, Serikali ya Marekani, kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), ilikabidhi pikipiki 16 za Yamaha na makabati 800 kwa ajili ya kuhifadhia faili zenye taarifa muhimu za walengwa, kwa Serikali ya Tanzania. Pikipiki hizi zitatumiwa na watoa huduma ngazi ya kata, kwa ajili ya kufuatilia utoaji wa huduma za jamii na afya kwa watoto na familia zilizo katika mazingira hatarishi. Wahudumu wa jamii wana vitendea kazi muhimu vinavyowawezesha kutoa rufaa kwenye huduma za upimaji na matibabu katika ngazi ya jamii. Makabati yatatumika kuhifadhi kumbukumbu za siri katika ngazi ya jamii.
Wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa, V. Kate Somvongsiri, Makamu Mkurugenzi Mkazi wa USAID alisema, “Wahudumu wa jamii ni vinara walio katika mstari wa mbele, na juhudi za pamoja ndizo zitakazosaidia kuweka vizazi vijavyo huru visipatwe na maambukizi ya UKIMWI”.
Kwa kuongezea, Serikali ya Marekani ilikabidhi seti 15,800 za vitabu zenye fomu maalum za ukusanyaji taarifa na takwimu zinazowezesha usimamizi bora wa taarifa za watoto wa Tanzania walio katika mazingira hatarishi zaidi pamoja na kaya zao. Mfumo huu wa ukusanyaji taarifa utasaidia kuboresha utoaji na ufuatiliaji wa taarifa za rufaa zilizotolewa kwa wateja pamoja na huduma za ustawi wa jamii na kinga. Pia, fulana 7,200 zilitolewa kwa wahudumu wa ngazi ya jamii pamoja na wasimamizi wao kama utambulisho wanapokuwa wanafanya ziara katika ngazi ya kaya kwa ajili ya kufuatilia maendeleo ya huduma inayotolewa kwa walengwa.
Pikipiki na vifaa vya ziada vilikabidhiwa Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), iliyowakilishwa na Waziri Selemani Jafo.
USAID, kupitia Mradi wa Kuimarisha Mifumo ya Afya ya Ustawi wa Jamii (CHSSP), inafanya kazi kwa karibu na Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Kusudi la ushirikiano huu ni kuhakikisha janga la VVU Tanzania linadhibitiwa kwa kuimarisha mifumo ya ustawi wa jamii kwa makundi yanayoishi katika mazingira hatarishi.