Mradi Maalum wa Serikali ya Marekani Kuwasaidia Wasichana Wengi Zaidi wa Kitanzania Kupata Elimu Bora

At the Mtakuja Secondary School in Dar es Salaam, USAID supports education through the provision of textbooks. The Let Girls Learn initiative in Tanzania will build on the country's educational progress to date, particularly for adolescent girls.
Mradi Maalum wa Serikali ya Marekani Kuwasaidia Wasichana Wengi Zaidi wa Kitanzania Kupata Elimu Bora
Mradi Maalum wa Serikali ya Marekani Kuwasaidia Wasichana Wengi Zaidi wa Kitanzania Kupata Elimu Bora

Nchi za Tanzania na Malawi zitapokea fedha kama nchi za kwanza za kipaumbele chini ya mradi maalumu wa kuwasaidia watoto wa kike kupata elimu bora ujulikanao kama “Let Girls Learn uliozinduliwa na Rais wa Marekani Barack Obama na mkewe, Mama Michelle Obama mwaka 2015.  Kwa hali hiyo, Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kuanzia tarehe 10 -12 Mei 2016 katika hoteli ya White Sands jijini Dar es Salaam, liliendesha warsha iliyowakutanisha wataalamu mbalimbali wa maendeleo ya kimataifa wa ndani na nje ya nchi, wafadhili na viongozi wa kiserikali kutoka Tanzania na Malawi ili kubuni kwa pamoja mikakati na mbinu zitakazowasaidia wasichana katika nchi hizi kupata elimu bora.

“Mradi huu unawaweka wasichana kama walengwa wakuu na kitovu cha jitihada zetu za kuboresha elimu na maendeleo duniani kote,” alisema Susan Markham,  Mratibu Mwandamizi wa Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake wa USAID. “Kwa kuelekeza jitihada zetu katika kushughulikia mahitaji maalumu ya wasichana, tunaweza kutatua kwa ufanisi zaidi vingi ya vikwazo vinavyowakwamisha wasiweze kupata elimu wanayostahili kuipata.”

Japokuwa nchini Tanzania  watoto wa kike na wa kiume huandikishwa katika shule za msingi kwa uwiano ulio sawa, kuna pengo kubwa baina yao katika kiwango chao cha kumaliza shule za sekondari. Miongoni mwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 20 na 24 ni aslimia 20 tu ya vijana wa kike ndio wameweza kumaliza elimu ya sekondari ikilinganishwa na zaidi ya asilimia 32 ya vijana wa kiume. Aidha, takwimu za Idadi ya Watu Kiumri na Afya ( Tanzania’s Demographic Health Survey Data) za mwaka 2010 zinaonyesha kuwa asilimia 20 ya wanawake katika umri huo hawakuwa na elimu kabisa ikilinganisha na chini ya asilimia 10 kwa wanaume.

Katika warsha hiyo washiriki walijadili kuhusu njia mbalimbali za kubadilisha mitazamo katika ngazi ya mtu mmoja mmoja, jamii na taasisi kuhusu thamani ya watoto wa kike;kujenga na kuimarisha mazingira yatakayowawezesha watoto wa kike kwenda shule; na kubaini njia za kuwawezesha watoto wa kike kufanya maamuzi kuhusu maisha yao na kutoa mchango muhimu katika jamii zao. Mikakati iliyoandaliwa katika warsha hii itakuwa msingi wa miradi ya baadaye katika nchi za Tanzania na Malawi katika kuwasaidia watoto wa kike kupata elimu bora kwa ufanisi na kujenga tabia zitakazowawezesha kuwa na afya njema.

Zaidi ya wasichana milioni 62 duniani kote hawaendi shule hivyo kuleta hasara kubwa kwa familia, jamii na nchi zao. Wasichana wanaokwenda shule hatimaye hupata kipato kikubwa zaidi, hupata watoto wakiwa katika umri mkubwa zaidi na wana uwezekano mdogo zaidi wa kupata maambukizo ya VVU/UKIMWI. Kila mwaka ambao mtoto wa kike anaendelea kubaki shuleni, kipato chake huongezeka kwa asilimia 25 na kupunguza uwezekano wa vifo vya watoto wachanga kwa hadi asilimia 10. Isitoshe, wanawake wenye elimu huwekeza asilimia 90 ya vipato vyao kwa familia zao na wana uwezekano wa zaidi ya mara mbili kuwapeleka watoto wao shule.

Mradi huu ni matokeo ya jitihada za serikali ya Marekani kwa ujumla wake ukijengwa na kuimarishwa  kupitia utaalamu na rasilimali za USAID, Ikulu ya Marekani, Shirika la Wafanyakazi wa Kujitolea wa Kimarekani (Peace Corps) na Wizara ya Mambo Nje ya Marekani. Aidha, warsha ya wiki hii inadhihirisha dhamira ya dhati  ya serikali ya Marekani  kusaidia maendeleo ya Tanzania na Malawi na kuziwezesha serikali zao kufikia malengo ya kuongeza upatikanaji na kukuza ubora wa elimu na mifumo yake na hatimaye kupata matokeo mazuri kielimu.

“Tunafahamu kuwa ukimuelimisha mtoto wa kike, unajenga familia yenye afya bora zaidi, unajenga jamii imara zaidi  na hatimaye taifa imara linaloweza kukabiliana kikamilifu na changamoto kadha wa kadha,” alisema Kaimu Mkurugenzi wa USAID nchini Tanzania Daniel Moore. “Ni kwa sababu hiyo uwekezaji katika kuboresha uwezo wa watoto wa kike kupata elimu ni uwekezaji muhimu zaidi tunaoweza kuufanya katika kuhakikisha maendeleo endelevu nchini Tanzania, Malawi na kwingineko duniani.”

Kwa taarifa zaidi kuhusu tukio hili, tafadhali wasiliana kwa barua pepe na Japhet Sanga (SangaJJ@state.gov), Afisa Habari Mwandamizi wa Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam.