Serikali Ya Marekani Yazindua Mradi Wa Dola Milioni 14.5 Wa Kulinda Mazingira, Kukuza Uhifadhi Na Utalii Nchini Tanzania

U.S. Ambassador Mark Childress and Natural Resources and Tourism Minister Lazaro Nyalandu shake hands at the launch of the PROTECT project, which took place yesterday at the Treetops Lodge in the Randilen Wildlife Management Area (Photo:U.S. Embassy, Dsm)
Balozi wa Marekani nchini Tanzania Mark Childress akipeana mkono na Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa kulinda mazingira na kukuza uhifadhi na utalii nchini Tanzania ujulikanao kama PROTECT.
Balozi wa Marekani nchini Tanzania Mark Childress akipeana mkono na Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa kulinda mazingira na kukuza uhifadhi na utalii nchini Tanzania ujulikanao kama PROTECT.

Jumatatu, tarehe 22 Juni, Serikali ya Marekani kwa kupitia Shirika lake la Ushirikiano wa Kimataifa (USAID) ilizindua rasmi mradi wa kulinda mazingira na kukuza uhifadhi na utalii nchini Tanzania ijulikanao kwa kifupi kama mradi wa PROTECT (Promoting Tanzania’s Environment, Conservation, and Tourism).  Uzinduzi huu ulifanyika katika hoteli ya Treetops Lodge iliyopo ndani ya eneo la hifadhi ya wanyamapori linalosimamiwa na jamii (WMA) la Randilen linalopakana na Hifadhi ya Taifa ya Tarangire ukiongozwa na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Mark Childress na Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali ya hifadhi wakiwemo askari wa wanyama pori wa kijiji cha Randilen.

PROTECT ni mradi wa miaka mitano utakaogharimu kiasi cha dola za Kimarekani milioni 14.5 utakaotekelezwa na taasisi iitwayo Engility/IRG.  Mradi huu unalenga kujenga uwezo wa uhifadhi na kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa wanyamapori nchini kote Tanzania.  Baadhi ya vipengele vya mradi huu vitalenga kuboresha sera na taasisi husika ili ziweze kusimamia kikamilifu maliasili ya wanyamapori, kuongeza ufanisi katika usimamizi wa sheria ikiwemo katika kuwakamata na kuendesha mashtaka dhidi ya majangili na wasafirishaji haramu wa wanyama pori pamoja na kuhimiza ushirikiano kati ya jumuiya za kiraia na serikali.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi, Balozi Childress alisema kuwa mradi wa PROTECT utalenga kutoa ufumbuzi wa muda mfupi kwa tatizo kubwa lililopo sasa la ujangili huku ukiweka misingi kwa mafanikio ya muda mrefu katika vita dhidi ya ujangili na usafirishaji haramu wa wanyamapori  pamoja na kuinua uhifadhi wa wanyamapori na bioanuai kwa ujumla.

 

Mradi wa PROTECT utazisaidia WMAs kwa kuzijengea uwezo na kuinua uwezo wa jamii zenyewe kusimamia rasilimali zao.  Hali kadhalika, utatoa ruzuku ndogo ndogo zitakazofikia jumla ya dola za Kimarekani milioni 2.75 katika kipindi cha miaka mitano.  Ruzuku hizi zitahamasisha mawazo mapya na ufumbuzi wa kibunifu katika kuboresha usimamizi wa wanyamapori; zitaimarisha uwezo wa wadau wakuu katika kutekeleza majukumu yao ya uhifadhi na kutoa motisha kwa wawekezaji binafsi katika biashara zinazohusu uhifadhi wa maliasili.

Mbali na mradi wa PROTECT, Balozi Childress alitangaza pia mradi mpya unaotarajiwa kuzinduliwa katika miezi ya hivi karibuni utakaoshughulikia maeneo na bayoanuai zilizo katika hatari ya kutoweka katika kanda ya Kaskazini mwa Tanzania.  Mradi huu wa miaka mitano utakaojulikana kama Endangered Ecosystems Northern Tanzania Project umetengewa fedha nyingine, kiasi cha dola za Kimarekani milioni 14 kwa ajili ya kuimarisha jitihada za kupambana na ujangili, kutoa misaada ya moja kwa moja kwa WMAs, jamii na wadau katika sekta ya utalii ili kuboresha usimamizi wa wanyamapori kaskazini kwa Tanzania.

Katika kuhitimisha hafla hiyo, Balozi Childress na Waziri Nyalandu walitia saini hati ya makubaliano ya kuanzisha miradi inayolenga kusaidia jitihada za Tanzania za kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa wanyamapori.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Afisa Habari Mwandamizi Japhet Sanga, Tel: 255-22-2294196, SangaJJ@state.gov