Serikali ya Marekani Yasaidia Asasi na Vikundi vya Kijamii Kuboresha Maisha ya Watanzania 30,000

Serikali ya Marekani Yasaidia Asasi na Vikundi vya Kijamii Kuboresha Maisha ya Watanzania 30,000
Serikali ya Marekani Yasaidia Asasi na Vikundi vya Kijamii Kuboresha Maisha ya Watanzania 30,000
Serikali ya Marekani Yasaidia Asasi na Vikundi vya Kijamii Kuboresha Maisha ya Watanzania 30,000

Hapo tarehe 19 Septemba 2016, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Bi Virginia Blaser alikabidhi ruzuku kwa vikundi na mashirika ya kijamii 22 yanayofanya kazi ya kuboresha maisha ya Watanzania katika hafla iliyofanyika katika Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam. Inatarajiwa kuwa ruzuku hiyo itawanufaisha moja kwa moja zaidi ya watu 30000 katika mikoa 16 humu nchini na itaboresha huduma na fursa katika sekta za maji na usafi wa mazingira, afya, elimu na maendeleo ya kiuchumi.

Ruzuku hizi zinatolewa chini ya programu maalum ya Ubalozi wa Marekani ya kusaidia vikundi na mashirika ya kijamii (Community Grants Program) ambayo hutoa msaada wa moja kwa moja kwa miradi midogo inayolenga kuboresha maisha ya jamii husika kupitia Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Miradi ya Kujitegemea ya Jamii (Ambassador’s Special Self-Help Fund) na  Mfuko wa Balozi wa Kukabiliana na VVU/UKIMWI (Ambassador’s Fund for HIV/AIDS Relief). Mfuko wa Balozi wa kusaidia Miradi ya Kujitegemea ya Jamii hutoa ruzuku za moja kwa moja kwa mashirika na vikundi vya kijamii kwa ajili ya utekelezaji wa miradi inayolenga kunufaisha jamii za vijijini na mijini wakati ambapo Mfuko wa Balozi wa Kukabiliana na VVU/UKIMWI hutoa msaada mahsusi kwa jamii zilizoathiriwa zaidi au zilizo katika hatari zaidi ya kuathiriwa na VVU/UKIMWI.

Serikali ya Marekani Yasaidia Asasi na Vikundi vya Kijamii Kuboresha Maisha ya Watanzania 30,000
Serikali ya Marekani Yasaidia Asasi na Vikundi vya Kijamii Kuboresha Maisha ya Watanzania 30,000

“Nyuma ya kila ruzuku kuna mchango mkubwa wa muda, jitihada na kujitoa kwa moyo.  Hii inajitafsiri katika matokeo makubwa sana yanayotokana na miradi inayopewa ruzuku. Tunafahari kushirikiana na wabia wetu ambao wamechukua jukumu kubwa la kushughulikia masuala muhimu katika jamii zao,” alisema Kaimu Balozi Virginia Blaser.

Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Miradi ya Kujitegemea ya Jamii ulianzishwa mwaka 1965, wakati wa muhula wa kwanza wa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere. Kwa zaidi ya miaka 50  ruzuku zinazotolewa na mfuko huu zimesaidia taasisi na vikundi vya kijamii kutoka kila mkoa wa Tanzania kuboresha maisha ya Watanzania kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujenga shule, kuwezesha upatikanaji wa maji safi, matumizi ya nishati ya jua na uanzishaji wa miradi ya kuongeza kipato.

Mfuko wa Balozi wa Kukabiliana na VVU/UKIMWI ulianzishwa mwaka 2009 na hadi sasa umetoa ruzuku kwa vikundi vya kijamii 81 nchini Tanzania. Mifuko hii inaendeleza utamaduni wa ushirikiano kati ya raia wa Marekani na Tanzania.

Ruzuku kupitia Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Miradi ya Kujitegemea ya Jamii kwa mwaka 2016 zinatolewa kwa:

Africa Schoolhouse ya Mwanza ambayo itajenga nyumba ya mwalimu katika Shule ya Sekondari Milembe ambayo inajumla ya wanafunzi wasichana 320.

Community Secondary Education Support (COSES) ambayo itanunua vifaa vya maabara kwa ajili ya Shule ya Sekondari ya Shimbwe yenye jumla ya wanafunzi 421.

Elizabeth Economic and Social Welfare Initiative ambayo itanunua vifaa kwa ajili ya kuchimba kisima kirefu kitakachowahudumia wakazi 1,800 wa kijiji cha Bukore  huko Bunda.

High Life Social Works Organization (HILSWO), ambayo itanunua vifaa na kujenga vyoo kwa ajili ya Shule ya Msingi ya Makangaga huko Lindi yenye wanafunzi 499.

KIKUKWI (Mradi wa ufugaji kuku Kwizu) ambacho kitanunua vifaa kwa ajili ya mradi wao wa kuku huko mkoani Kilimanjaro unaowanufaisha wanawake 58.

Kikundi cha Kilimo Upendo Group cha mkoani Morogoro ambacho kitanunua mizinga ya nyuki na vifaa vingine vya ufugaji nyuki kwa manufaa ya wanachama wake 19.

Kilimo na Ufugaji Kanyezi (KIU) ambacho kitanunua na kufunga mashine ya kukamua mafuta kwa ajili ya wanachama wake 15 huko Rukwa.

Pemba Foundation, kwa kushirikiana na vyama vitatu vya ushirika huko Pemba, watanunua vifaa na kujenga mfumo wa umwagiliaji mashamba kwa matone (drip irrigation systems) katika vijiji vitatu na kunufaisha familia 56.

Kikundi cha Wanawake Tunaweza  cha mkoani Mbeya, ambacho kitanunua vifaa na kuchimba kisima kirefu kitakachowahudumia wananchi wapatao 2,600.

Women Caring for the Environment (WOCE) cha jijini Dar es Salaam, kitanunua vifaa vya usalama, kujikinga na kufanyia usafi vitakavyowanufaisha wanawake 20 wanaofanya kazi ya usafi na uzoaji takataka jijini.
Ruzuku kupitia mfuko wa Mfuko wa Balozi wa Kukabiliana na VVU/UKIMWI  zinatolewa kwa:

Kikundi cha Chakumuma cha Mtwara ambacho kitanunua vifaa na kujenga matanki matatu ya lita 25,000 kila moja kwa ajili ya kuvuna maji ya mvua kwa ajili ya shule 3 za msingi mkoani humo pamoja na kuwahudumia wananchi wapatao 1,500.

Foxes Community and Wildlife Conservation Trust (FCWCT) ya mkoani Iringa itahudumia zaidi ya watu 500 katika programu zake tatu. Wanapanga 1) Kununua maziwa ya kopo kwa ajili ya watoto wachanga yatima; 2) kununua vifaa vya kufundishia na vifaa vingine kwa ajili ya shule ya awali na 3) kujenga mabanda mawili ya kuendeshea kilimo cha kitaalamu (greenhouses), kujenga banda moja la mifugo na kununua mifugo kwa ajili ya kutolea mafunzo ya kukuza stadi za vijana waliopo katika mazingira hatarishi.

Hope 4 Young Girls Tanzania ambao watanunua vitanda, matandiko na taulo za kike kwa wanafuzi 139 katika shule ya yatima ya Hananasif iliyopo Mkuranga, Dar es Salaam.

Kwa Wazee ya mkoa wa Kagera ambayo itatumia ruzuku kutoa mafunzo kwa wavulana wapatao 350 kuhusu programu yao iitwayo ‘amani ni uchaguzi’ (‘Peace is a Decision’) inayolenga kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya wasichana na wanawake.

Hospitali ya Walutheri ya Lugala ambayo itanunua na kufunga vifaa vya umeme jua pamoja na taa zake katika dispensari ya Tanganyika-Masagati Dispensary, Morogoro inayowahudumia wagonjwa 3,881 kwa mwaka.

Kikundi cha Matumaini Group cha Kigoma  ambacho kitanunua magodoro na mashuka kwa ajili ya kituo cha afya cha Mabamba huko Kibondo.

Kijiji cha Mavuno cha Mwanza kinapanga kutumia ruzuku kununua na kufunga pampu ya maji inayotumia nishati ya jua katika kituo cha watoto yatima kijijini Mavunona hivyo kuwahudumia watoto na wafanyakazi wa kituo wapatao 155.

Molly’s Network itatoa mafunzo ya kuzijengea uwezo (capacity building training) kwa asasi 6 zinafanya kazi na walengwa wapatao 4,800 ambao ni watu walio katika hatari ya kuambukizwa VVU na wale wanaoishi na VVU/UKIMWI jijini Dar es Salaam.

Mtwara Youth Anti AIDS Group (MYAAG) ambacho kitanunua cherehani na vifaa vingine vya ushonaji kwa ajili ya mafunzo ya vijana 40 katika wilaya ya Mtwara.

The Registered Trustees of Share and Care Foundation ambao watanunua vifaa na kujenga matanki ya kuvunia maji ya mvua katika shule 10 mkoani Tanga hivyo kuwanufaisha watu 11,785 wakiwemo wanafunzi, walimu, wafanyakazi wa shule na wanajamii wanaozunguka shule hizo. 

Nyumba ya Watoto yatima ya mkoani Kilimanjaro itanunua mabomba, matanki na vifaa vingine kwa ajili ya mradi wa maji utakaowahudumia watu 1,400 wakiwemo wakazi wa Nyumba hiyo na jamii inayoizunguka.

Women and Child Vision (WOCHIVI)  ya mkoani Arusha itanunua vifaa na kujenga vyoo katika shule ya msingi ya Olkerian vitakavyowahudumia wanafunzi 876 pamoja na walimu na wafanyakazi wa shule.

___________________________________________________

Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Miradi ya Kujitegemea ya Jamii na Mfuko wa Balozi wa Kukabiliana na UKIMWI ni sehemu ya programu ya Balozi wa Marekani ya kutoa ruzuku kwa miradi mbalimbali ya kijamii. Kwa maelezo zaidi kuhusu programu hii kufahamu, tafadhali tembelea tovuti ya Ubalozi wa Marekani au wasiliana na Afisa wa Ubalozi Anayeshughulikia Ruzuku kwa anuani ya barua pepe selfhelpd@state.gov au kwa barua kupitia S.L.P 9123, Dar es Salaam.