Dar es Salaam — Kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) limezindua mradi mpya wa kuimarisha uwezo wa vituo vya afya, watumishi wa afya, viongozi wa dini na watu wenye ulemavu kukabiliana na janga la UVIKO-19. Hafla ya uzinduzi wa mradi wa Pambana na Uviko-19 imefanyika leo jijini Dar na Balozi wa Marekani nchini, Waziri Mkuu wa Tanzania, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar-es-Salaam, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania wakihudhuria.
Serikali ya Marekani kupitia USAID imetoa Dola za Marekani 550,000 kwa TEC kutekeleza mradi wa Pambana na Uviko-19. Kwa madhumuni ya kuunga mkono juhudi za kitaifa za kukabiliana na janga la UVIKO-19, kuwezesha ununuzi wa vifaa vya matibabu kama vile mitungi ya oksijeni, vifaa vya ufuatiliaji wa wagonjwa, na mashine ndogo za kutengeneza oksijeni katika hospitali 12 za Dar es Salaam, Kagera, Bukoba, Kigoma, Mbeya, Morogoro, Ruvuma, Arusha, Kilimanjaro, Singida, Mtwara na Iringa.
Pambana na UVIKO-19 itaongeza ujuzi wa wafanyakazi wa afya ili kuboresha usimamizi wa wagonjwa wa UVIKO-19 na kusaidia usimamizi wa chanjo za UVIKO-19 katika mikoa 12 sanjari na miongozo ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto (WAMJW) na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Baraza la Maaskofu limeeleza ufadhili huo unakuja kwa wakati muafaka kwani virusi vya UVIKO-19 vinaendelea kuathiri maisha ya Watanzania wengi. Uwekezaji katika vifaa muhimu vya kuokoa maisha na mafunzo kwa watumishi wa afya utaimarisha uwezo wa hospitali zilizopo chini ya Baraza la Maaskofu kukabiliana na wagonjwa ambao wana dalili hatarishi za kutishia maisha kutokana na virusi vya UVIKO-19. “Tunalipongeza Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kwa kuunga mkono uhamasishaji wa chanjo ya UVIKO-19 katika kuokoa maisha ya watu. Mradi huu utahakikisha watu wengi wanapata elimu sahihi na kupata chanjo”, Askofu Mkuu Jude Thaddaeus Ruwai’chi wa jimbo Kuu la Dar es Salaam alisema.
Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dkt. Donald Wright amesema, “ingawa harakati za kupunguza athari za UVIKO-19 ni muhimu, njia sahihi ya kukabiliana na janga hili ni kudhibiti virusi kabla ya kuambukiza watu. Kuenea kwa chanjo ulimwenguni ndio njia bora zaidi ya kumaliza janga hili”. Balozi alisisitiza kujitolea kwa Serikali ya Marekani kupunguza UVIKO-19 kupitia njia zilizoratibiwa na kuwahimiza waliohudhuria kuhakikisha wanapata chanjo na kueneza ujumbe kwamba chanjo ni salama na ina ufanisi na inatoa matumaini makubwa ya kupambana na UVIKO-19 hapa nchini Tanzania na ulimwenguni kote.