Askari wa Marekani Watoa Mafunzo kwa Askari wa Wanyamapori Selous

A U.S. Marine training Selous Park Rangers on patrolling techniques. The training is being conducted by U.S. Marines and Sailors from March 2-27 in the Selous Game Reserve. (Photo: U.S. Embassy, Dar es Salaam)
Askari wa Marekani Watoa Mafunzo kwa Askari wa Wanyamapori Selous (Picha kwa hisani ya Ubalozi wa Marekani, Dar es Salaam)
Askari wa Marekani Watoa Mafunzo kwa Askari wa Wanyamapori Selous (Picha kwa hisani ya Ubalozi wa Marekani, Dar es Salaam)

Hifadhi ya Wanyamapori Selous, TANZANIA.  Jumatatu wiki hii, Balozi Mark Childress alikuwa katika Hifadhi ya Wanyamapori ya Selous akishuhudia mafunzo yanayotolewa na Askari wa Majini na Nchi Kavu wa Jeshi la Marekani kwa Askari wa Wanyamapori wapatao 50 katika hifadhi hiyo.  Mafunzo haya yatakayochukua mwezi mmoja yanalenga kuwawezesha askari hao wa wanyamapori kupambana kikamilifu na vitendo vya kihalifu katika hifadhi hiyo.  Wakufunzi wa Kimarekani wanaotoka katika kikosi maalumu cha askari wa miguu, wanamaji na wanaanga cha kukabiliana na Majanga Barani Afrika wanasaidia kuwajengea uwezo askari wa wanyamapori kwa kuwafundisha mbinu za medani wakiwa katika kikundi kidogo (small unit tactics), mbinu za doria, operesheni nyakati za usiku na masuala  ya lojistiki ili kuongeza ufanisi wao katika hifadhi.

Katika ziara yake hiyo, Balozi Childress alishuhudia mafunzo ya darasani na yale ya vitendo kuhusu  mbinu za doria.  Aidha, alielezea kuhusu sifa nzuri ambazo wanajeshi wa Kimarekani wamejijengea nchini Marekani na ushirikiano wao wenye mafanikio na Askari wa Wanyamapori wa Kitanzania.  Alielezea kufurahishwa kwake na jinsi mafunzo hayo yalivyokuwa yakiendeshwa na kusisitizia dhamira ya dhati ya Marekani ya kuwasaidia askari wa wanyamapori katika jitihada za kudhibiti usafirishaji haramu wa maliasili hii.

Askari wa Marekani Lance Cpl. Kyle McAuliffe atoa Mafunzo kwa Askari wa Wanyamapori Selous (Picha kwa hisani ya Askari wa Marekani Lance Cpl. Lucas J. Hopkins)
Askari wa Marekani Lance Cpl. Kyle McAuliffe atoa Mafunzo kwa Askari wa Wanyamapori Selous (Picha kwa hisani ya Askari wa Marekani Lance Cpl. Lucas J. Hopkins)

Baada ya awamu hii ya mafunzo kukamilika, wakufunzi wa Kimarekani watarejea tena Tanzania kwa awamu nyingine ya mafunzo itakayofanyika baadaye mwaka huu. Mbali na mafunzo ya kijeshi, Serikali ya Marekani inatoa pia mafunzo kuhusu masuala mengine mbalimbali kama vile namna ya kukabiliana na utakatishaji fedha na uendeshaji wa mashtaka wenye ufanisi dhidi ya majangili na wale wanaojihusisha na usafirishaji haramu wa wanyamapori.  Mwezi Januari mwaka huu, Marekani na Ujerumani walikabidhi vifaa mbalimbali vitakavyotumiwa na askari wa wanyamapori katika shughuli zao za doria katika hifadhi. Vifaa hivyo ni pamoja na mahema makubwa na madogo, kurunzi zenye mwanga mkali, ramani, darubini, kamera, sare na viatu.  Misaada hii ni sehemu ya programu kubwa ya kusaidia jitihada za Tanzania za kukabiliana na usafirishaji haramu wa wanyamapori na uhifadhi itakayogharimu Dola za Kimarekani milioni 40 katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Aidha, msaada huu unatolewa sambamba na jitihada za wadau wengine wa kimataifa kama vile taasisi iitwayo Paul Allen Foundation, ambayo imegharimia mfumo mpya wa mawasiliano (VHF system) unaowawezesha askari wa wanyamapori kuwasiliana vyema na kuratibu shughuli zao za kukabiliana na ujangili bila mawasiliano yao kuingiliwa.

Kwa taarifa zaidi  kuhusu tukio hili, tafadhali wasiliana na Japhet Sanga (SangaJJ@state.gov), Afisa Habari Mwandamizi, Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam.