Flag

An official website of the United States government

Kamanda wa Jeshi na Marekani atembelea maabara zinazofadhiliwa na Taasisi ya Utafiti ya Walter Reed
na Vituo vya Afya vya Jeshi la Wananchi Tanzania
5 MINUTE READ
Aprili 11, 2022

Dar es Salaam, Tanzania – Wiki iliyopita Kamanda wa Taasisi ya Utafiti wa Kijeshi ya Walter (WRAIR), Kanali Chad Koenig, alitembelea hospitali na vituo kadhaa vya afya pamoja na maabara za uchunguzi na utafiti nchini Tanzania. WRAIR ikijulikana pia kama Taasisi ya Walter Reed, ni taasisi ya serikali ya Marekani inayoendesha shughuli zake katika Wizara ya Ulinzi. WRAIR imekuwa ikiendesha shughuli zake nchini Tanzania toka mwaka 1999. Lengo kuu la Walter Reed nchini Tanzania ni kutokomeza janga la VVU kupitia utafiti na utekelezaji wa programu za kinga, huduma na matibabu ya VVU zinazofadhiliwa na PEPFAR. Hii ilikuwa ziara ya kwanza ya Kamanda Koenig nchini Tanzania ambapo amesifu ubora wa hospitali na vituo vya afya alivyovitembelea na ubora wa huduma zinazotolewa kwa wagonjwa. “Nimevutiwa sana na kiwango cha huduma mnazozitoa, hata katika mikoa ya pembezoni zaidi ya Tanzania,” alisema.

Walter Reed inaelekeza shughuli zake za kukabiliana na VVU katika mikoa mitano ya Nyanda za Juu Kusini: Mbeya, Rukwa, Katavi, Songwe na Ruvuma. Katika maeneo haya, WRAIR, kupitia mbia wake wa utekelezaji miradi, Henry M. Jackson Foundation for Medical Research International (HJFMRI), inatoa huduma mtambuka na kamilifu za matunzo na matibabu ya VVU/UKIMWI. Kwa ufadhili kutoka Serikali ya Marekani, HJFMRI inatoa huduma za matibabu ya dawa za kufubaza VVU kwa watu 210,000 wanaoishi na VVU.

Ziara ya Kamanda Koenig na ujumbe wake, uliomjumuisha Afisa Mkuu wa Utafiti wa Kisayansi wa Walter Reed Dk. Karen Peterson, na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Utafiti wa Tiba wa Jeshi la Marekani Kamandi ya Afrika, Kanali Shannon Lacy, iliangazia programu za utafiti za Walter Reed nchini Tanzania. Akiwatembelea wabia kutoka taasisi ya PharmAccess International ya jijini Dar es Salaam, inayoendesha Programu ya Walter Reed ya utafiti wa maradhi mapya ya kuambukiza (Global Emerging Infectious Diseases Program), Dk. Peterson aliahidi kwamba Marekani itaendelea kuifadhili programu hii. Alisema, “Nimefurahi kusikia kwamba kuna andiko la mradi (proposal) la kuendelea na kazi hii muhimu. Tutaendelea kuufuatilia mradi huu na kuhakikisha kuwa unaendelea.”

Hali kadhalika, ujumbe wa Kamanda Koenig ulitembelea Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya iliyopo Nyanda za Juu Kusini kuangalia maabara za utafiti zinazofadhiliwa na Walter Reed ikiwa ni pamoja na maabara za Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Maradhi ya Binadamu (NIMRI) – Kituo cha Utafiti cha Mbeya na maabara zinazoendeshwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na HJFMRI. Maabara hizi ni zile za uchunguzi wa Kifua Kikuu, maabara za kliniki za majaribio ya chanjo za VVU, maabara za kupima wingi wa VVU na mabadiliko yake (HIV viral load and sequencing facilities), maabara za UVIKO-19 na tafiti za muda mrefu za kuwafuatilia watu wanaoishi na VVU barani Afrika toka mwaka 2008 ili kuiwezesha serikali kuandaa sera na programu mbalimbali za kukabiliana na janga hili. Akizungumzia ushirikiano huu wa zaidi ya miaka 20, Kanali Koenig alisema, “Tunatumaini kuwa kupitia msaada wetu kwa shughuli za utafiti nchini Tanzania, tutaweza kuiweka nchi hii mahali pazuri zaidi kupambana vyema zaidi sio tu na VVU bali pia maradhi mengine ya mlipuko yanayoweza kujitokeza katika siku zijazo.”

Ujumbe wa Kamanda Koenig ulimazia ziara yake kwa kutembelea Hospitali Kuu ya Kijeshi ya Lugalo ambapo ulikutana na wawakilishi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Kiongozi Mkuu wa Huduma za Matibabu na Kamanda wa Hospitali ya Lugalo, Brigedia Jenerali Dk. Agatha Katua. Toka mwaka 2006, Serikali ya Marekani, kupitia Walter Reed, imekuwa ikiisaidia programu ya huduma na matibabu ya VVU/UKIMWI ya JWTZ na hivi sasa inasaidia jumla ya hospitali na vituo vya afya vya JWTZ vipatavyo 21 nchini kote Tanzania. Katika kila hospitali na kituo cha afya miongoni mwa vituo hivi, askari, familia zao na jamii inayozunguka wanapatiwa huduma za ushauri nasaha kuhusu VVU, upimaji wa VVU, mbinu za kujilinda dhidi ya maambukizi, matibabu ya dawa za kufubaza VVU, kuzuia maambukizi toka kwa mama kwenda kwa mtoto pamoja na miradi ya kusaidia watoto yatima na walio katika mazingira magumu.