Ubalozi Wa Marekani Kushirikiana Na Tamasha La Kimataifa La Filamu La Zanzibar (ZIFF) Katika Programu Ya Mabadilishano Ya Kitamaduni

Signing of a Memorandum of Understanding (MOU) between the Zanzibar International Film Festival (ZIFF) and the U.S. Embassy to facilitate the participation of two American film experts in ZIFF this July, 2017.

Signing of a Memorandum of Understanding (MOU) between the Zanzibar International Film Festival (ZIFF) and the U.S. Embassy to facilitate the participation of two American film experts in ZIFF this July, 2017.

Dar es Salaam, TANZANIA. Tarehe 17 Mei, Ubalozi wa Marekani uliingia rasmi katika ubia na Tamasha la Kimataifa la Filamu Zanzibar kwa kusaini Hati ya Makubaliano  (MOU) ya kuwa na programu ya mabadilishano ya kitamaduni ya wiki moja itakayohusisha kuwaleta nchini Tanzania Mwongozaji wa Filamu wa Kimarekani Judd Ehrlich na mtaalamu wa filamu Debra Zimmerman kutoka tarehe 9 hadi16 Julai, 2017.  Hati hiyo ya Makubaliano ilisainiwa na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Virginia Blaser na Mkurugenzi wa  ZIFF Fabrizio Colombo.

Judd Ehrlich ni muongozaji wa filamu ya maisha na matukio halisia (documentary) iitwayo  Keepers of the Game, ambayo inaangazia jitihada za timu ya wasichana kutoka makabila ya asili ya Marekani ikitafuta kushinda ubingwa wa mkoa wa mchezo uitwao  lacrosse, ambao kitamaduni ulikuwa ni mchezo wa wanaume na wavulana tu.  Debra Zimmerman ni mtaalamu wa filamu na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi iitwayo Women Make Movies (Wanawake Watengeneza Filamu) ambayo imedhamiria kuongeza uwezo na fursa kwa wanawake wanaohusika katika utengenezaji wa filamu.

Kupitia ubia na ZIFF, Ehrlich na  Zimmerman watafanya kazi moja kwa moja na watengeneza filamu wa Kizanzibari wanaochipukia wakati wa tamasha la 20 la filamu la Zanzibar. Wataendesha warsha kadhaa kuhusu utengenezaji wa filamu za maisha na matukio halisia na utafutaji masoko na usambazaji wa filamu pamoja na kuendesha warsha mahsusi kuhusu ushiriki wa wanawake katika tasnia ya filamu.

Akizungumza katika hafla fupi ya kusaini Hati ya Makubaliano, Kaimu Balozi Blaser alisema “tunafuraha kuimarisha msaada wetu kwa watu wa Zanzibar kupitia programu hii ya mabadilishano ya kitamaduni.  Kwa pamoja tutatoa fursa kwa watengeneza filamu wa Kimarekani na Kizanzibari kutumia sanaa hii kama nyezo ya kushughulikia masuala mbalimbali yanayogusa jamii zao.”

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Ofisi ya Habari ya Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam kwa simu namba: +255 22 229-4000 au kwa barua pepe: DPO@state.gov.