Ubalozi Wa Marekani Na Serikali Ya Tanzania Kukabidhi Miradi Ya Maji Mikoa Ya Morogoro Na Iringa

Oktoba 30, 2018, Serikali ya Tanzania na Serikali ya Marekani, kupitia Shirika la Marekani la Misaada ya Maendeleo ya Kimataifa (USAID), wamekabidhi miradi ya kusambaza maji kwa jamii katika kijiji cha Msowero katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Mkoa wa Morogoro. Mradi huu ni sehemu ya mpango mpana wa kuboresha mifumo ya maji katika mikoa ya Morogoro na Iringa. Utatoa maji safi ya kunywa kwa takribani watu 14,000.

The Water Resources Integration Development Initiative (WARIDI) ni mradi wa miaka mitano, wa shilingi za Kitanzania bilioni 5.5 unaofadhiliwa na USAID. Kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya na jamii, WARIDI imetekeleza miradi 16 ya kusambaza maji kati ya Novemba 2017 na Oktoba 2018. Mradi umesaidia kujenga uwezo wa mashirika ya maji kwa jamii ili kuhakikisha huduma za kudumu zinawasilishwa kwa wanufaikaji wote. Miradi 16 ya kusambaza maji huhudumia zaidi ya watu 169,000. Miradi ya maji 34 ya ziada iko kwenye mchoro na itajengwa na WARIDI kati ya 2019 na 2021.

WARIDI ilipokea michango muhimu na msaada kutoka kwa jamii pamoja na msaada wa Serikali ya Tanzania. Michango ya jamii kwa ajili ya miradi iliyofikia zaidi ya shilingi za Kitanzania milioni 750. Mradi huu unaonesha ushirikiano thabiti na wa wazi kati ya Serikali ya Marekani na Serikali ya Tanzania kusaidia Mradi wa Maendeleo wa Sekta ya Maji (WSDP II) wa Wizara ya Maji Tanzania.

Miradi inaruhusu watu wa vijijini kupata maji safi kwenye umbali mfupi, kupunguza mzigo kwa wanawake na watoto wa kike ambao mara nyingi huhitajika kukusanya maji kutoka vyanzo visivyo salama mbali na nyumbani. Mradi wa USAID WARIDI pia unasaidia kuboresha usafi wa mazingira na maisha ya wananchi katika ngazi ya wilaya na jamii.