Ubalozi wa Marekani Unampongeza Maxence Melo kwa kutunukiwa Tuzo ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari

Maxence Melo Mubyazi (Phicha kwa hisani ya Jamii Forums)

Dar es Salaam: Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania unampongeza Maxence Melo, kwa kutangazwa mmoja wa washindi wa Tuzo ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari kwa mwaka 2019, tuzo inayotolewa na Kamati ya Ulinzi kwa Waandishi wa Habari. Pamoja na kukabiliwa na changamoto nyingi za kisheria, Maxence Melo na Jamii Forums wameendelea kuwa mstari wa mbele katika kutetea uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania. Tanzania inajivunia historia kubwa iliyosheheni mchango mkubwa wa vyombo vya habari, kuanzia mchango wa Radio Tanzania Dar es Salaam katika ukombozi wa Afrika, kuimarisha umoja wa Afrika na kukuza amani na haki.

Kutambuliwa kwa Maxence Melo  na kutunukiwa kwake tuzo hii kunatukumbusha urithi huu muhimu wa historia ya nchi hii; urithi ambao unatishiwa pale ambapo matukio ya  ukiukwaji wa haki, unyanyasaji na hata watu kupotea zinapogubika utamaduni wa maendeleo ya kijamii yanayosukumwa na vyombo vya habari. Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania unatoa wito kwa Serikali ya Tanzania kulinda urithi huu wa kihistoria kwa kuimarisha usalama wa waandishi wa habari na kutokomeza hali ya wale wanaowadhuru kutokuchukuliwa hatua zinazostahili.