Ubalozi Wa Marekani Waendesha Mahafali Ya Washiriki Wa Programu Ya Mafunzo Ya Kiingereza Dar es Salaam

Dar es Salaam, TANZANIA. Tarehe 14 Septemba, Afisa wa Ubalozi wa Marekani anayeshughulikia masuala ya umma Bi. Brinille Ellis aliwakaribisha wanafunzi, wazazi na walimu zaidi ya 100 katika Shule ya JOMAK School iliyopo huko Bahari Beach katika mahafali ya washiriki wa programu ya mafunzo ya Kiingereza inayofadhiliwa na Ubalozi iitwayo “English Access Microscholarship Program”. Wanafunzi wapatao 25 wa vidato vya tatu, nne na tano walianza kuhudhuria mafunzo yao ya Kiingereza baada ya masomo ya kawaida shuleni katika shule ya JOMAK hapo mwezi Septemba mwaka 2015. Hawa watakuwa kundi la kwanza la wahitimu wa programu hii jijini Dar es Salaam. Serikali ya Marekani inafadhili madarasa mengine matatu hapa nchini chini ya programu hii. Hii ni pamoja na darasa la pili katika shule ya JOMAK na madarasa mawili mjini Moshi yanayoendeshwa na taasisi iitwayo Kilimanjaro Information Technology. Inatarajiwa kuwa madarasa mengine yataanza mwezi Januari 2018 katika miji ya Mwanza, Tanga and Zanzibar.

Bi. Ellis aliwapongeza wanafunzi wa programu hii kwa kujitoa kwao kwa dhati na kushiriki kikamilifu katika mafunzo yao: “Kwa kupitia programu ya Access mmepata mambo mengi zaidi ya ujuzi wa lugha ya Kiingereza. Mmekuwa viongozi wa jamii na mfano wa kuigwa katika jamii zenu.” Wakati wa hafla hii, wanafunzi walifanya maonyesho na kutambulisha kwa Kiingereza miradi na kazi mbalimbali za kuhudumia jamii walizozifanya wakati wa mafunzo yao katika programu hii.

Programu ya Access hutoa mafunzo ya msingi ya lugha ya Kiingereza kwa watoto na vijana wenye vipaji wa kuanzia miaka 13 hadi 20 kutoka jamii zenye hali duni kiuchumi kupitia madarasa yanayoendeshwa baada ya muda wa shule na yanayotoa mafunzo ya kina. Programu ya Access huwapatia washiriki wake stadi za lugha ya Kiingereza jambo ambalo huwapa fursa zaidi za kielimu na ajira. Toka mwaka 2004, zaidi ya wanafunzi 200 kutoka Tanzania na 100,000 kutoka zaidi ya nchi 85 wameshiriki katika programu hii. Kwa maelezo zaidi, tembelea: https://americanenglish.state.gov/.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Ofisi ya Habari ya Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam kwa simu namba: +255 22 229-4000 au kwa barua pepe: DPO@state.gov.